Agano la Kale

Agano Jipya

Ezekieli 20:30-43 Biblia Habari Njema (BHN)

30. Basi, waambie Waisraeli kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nawauliza hivi: Je, mtajitia unajisi kwa kufuata desturi za wazee wenu na kuviabudu vitu vinavyonichukiza?

31. Mnapoendelea kutoa tambiko zenu na kuwapitisha watoto wenu motoni mnajitia unajisi mpaka leo hii. Je, nitaulizwa shauri nanyi, enyi watu wa Israeli? Lakini, kama niishivyo, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu naapa kwamba sitakubali kuulizwa shauri nanyi.

32. Nyinyi mnasema mioyoni mwenu, ‘Tutakuwa kama mataifa mengine, kama makabila ya nchi nyingine na kuabudu miti na mawe.’ Hayo mnayopania mioyoni mwenu hayatafanikiwa kamwe.

33. “Kama niishivyo mimi Bwana Mwenyezi-Mungu, naapa kwamba mimi nitawatawala kwa mkono wenye nguvu, kwa ukali na kuwamwagia ghadhabu yangu.

34. Nitawatoa kutoka mataifa na kuwakusanya kutoka nchi mlikotawanywa kwa mkono wangu wenye nguvu, kwa ukali na kwa ghadhabu yangu.

35. Nitawapeleka kwenye jangwa la mataifa; na huko nitawahukumu moja kwa moja.

36. Kama nilivyowahukumu wazee wenu kule jangwani katika nchi ya Misri, ndivyo nitakavyowahukumu nyinyi. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.

37. “Nitawalazimisha muwe chini ya uchungaji wangu kila mmoja, na kuwafanya mlitii agano langu.

38. Nitaondoa miongoni mwenu waasi na wale wanaonikosea; nitawaondoa katika nchi walikokaa kama wakimbizi, lakini nchi ya Israeli hawataiingia kamwe. Hapo ndipo mtakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.

39. “Na sasa, enyi Waisraeli, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nawaambia hivi: Haya! Endeleeni kuziabudu sanamu zenu za miungu, kama hamnisikilizi; lakini mtalazimika kuacha kulikufuru jina langu takatifu kwa tambiko na sanamu zenu.

40. Maana, katika mlima wangu mtakatifu, mlima mrefu wa Israeli, natamka mimi Bwana Mwenyezi-Mungu, nyinyi nyote watu wa Israeli mtanitumikia huko. Huko mimi nitawapokeeni na kungojea mniletee huko sadaka na tambiko zenu bora na matoleo mliyoyaweka wakfu.

41. Baada ya kuwatoa katika nchi ambako mmetawanywa na kuwakusanya pamoja, nitazipokea tambiko zenu za harufu nzuri. Nami nitadhihirisha utakatifu wangu kati yenu mbele ya mataifa mengine.

42. Nanyi mtatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu, wakati nitakapowaleta mpaka katika nchi ya Israeli, nchi niliyoapa kuwapa wazee wenu.

43. Huko ndiko mtakapokumbuka mwenendo wenu na matendo yenu mabaya ambayo yaliwatieni unajisi; nanyi mtachukizwa kabisa kwa sababu ya maovu yote mliyotenda.

Kusoma sura kamili Ezekieli 20