Agano la Kale

Agano Jipya

Ezekieli 20:24-31 Biblia Habari Njema (BHN)

24. kwa sababu hawakufuata amri zangu, bali walizikataa kanuni zangu, wakazikufuru Sabato zangu na kuziabudu sanamu za miungu ya wazee wao.

25. “Tena niliwapa kanuni mbaya na amri ambazo mtu akizifuata hataishi.

26. Nikawaacha watiwe unajisi kwa tambiko zao za kuwatoa wazaliwa wao wa kwanza kafara kwa sanamu za miungu. Hili lilikuwa pigo lao la adhabu ya kutisha ili watambue kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.

27. “Sasa, wewe mtu, waambie Waisraeli kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema: Wazee wenu walinikufuru kila mara kwa kukosa uaminifu.

28. Maana nilipowapeleka katika ile nchi niliyoapa kuwapa, kila walipoona kilima kirefu au miti ya majani mengi, walianza kutoa matambiko na tambiko zao na kunichokoza. Hukohuko walitoa tambiko za harufu nzuri na kumimina tambiko za kinywaji.

29. (Mimi nikawauliza, ‘Mahali hapo palipoinuka mnapokwenda panaitwaje?’ Wao wakapaita ‘Mahali palipoinuka’ mpaka leo.)

30. Basi, waambie Waisraeli kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nawauliza hivi: Je, mtajitia unajisi kwa kufuata desturi za wazee wenu na kuviabudu vitu vinavyonichukiza?

31. Mnapoendelea kutoa tambiko zenu na kuwapitisha watoto wenu motoni mnajitia unajisi mpaka leo hii. Je, nitaulizwa shauri nanyi, enyi watu wa Israeli? Lakini, kama niishivyo, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu naapa kwamba sitakubali kuulizwa shauri nanyi.

Kusoma sura kamili Ezekieli 20