Agano la Kale

Agano Jipya

Ezekieli 12:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Neno la Mwenyezi-Mungu likanijia:

2. “Wewe mtu! Wewe unakaa kati ya watu waasi. Wana macho lakini hawaoni; wana masikio lakini hawasikii.

3. Wao ni watu waasi. Basi, ewe mtu, fanya kama vile unakwenda uhamishoni: Ondoka wakiwa wanakuona, ukimbilie mahali pengine. Nenda kama mkimbizi kutoka mahali ulipo mpaka mahali pengine wao wakikuona. Labda wataelewa, ingawa wao ni waasi.

4. Hakikisha wanaona unachofanya. Funga mzigo wako uutoe nje na kuwa tayari kuondoka jioni kama wafanyavyo watu wanaokwenda uhamishoni.

5. Wakiwa wanakuangalia toboa ukuta wa nyumba, upitie hapo na kwenda nje.

6. Wakiwa wanakuona, jitwike mabegani mzigo wako na kuondoka wakati wa giza. Funika uso wako usiweze kuona unakwenda wapi. Ndivyo ninavyokufanya uwe ishara kwa Waisraeli.”

7. Basi, nikafanya kama nilivyoamriwa. Siku hiyo, wakati wa mchana, nikafunga mzigo wangu kama mzigo wa mtu anayekimbia. Jioni nikautoboa ukuta na giza lilipokuwa likiingia, nikatoka, nimejitwika mzigo wangu mabegani, watu wote wakiniona.

8. Kesho yake asubuhi, Mwenyezi-Mungu akaniuliza:

9. “Wewe mtu! Je, hao waasi wa Israeli hawajakuuliza maana ya hicho ulichofanya?

10. Waambie kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema: Kauli hii yangu yahusu mambo yatakayompata mtawala wa Yerusalemu na watu wote wa Israeli wanaoishi humo.

11. Waambie kuwa wewe ni ishara kwao; kama ulivyofanya ndivyo itakavyotendeka kwao: Watakwenda uhamishoni; naam, watachukuliwa mateka.

Kusoma sura kamili Ezekieli 12