Agano la Kale

Agano Jipya

Esta 9:1-16 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili, yaani mwezi wa Adari, ilipofika, siku ambayo tangazo la mfalme lingetekelezwa, na maadui wa Wayahudi walitarajia kuwashinda Wayahudi, iligeuzwa kuwa siku ya ushindi kwa Wayahudi dhidi ya adui zao.

2. Katika kila mji wa kila mkoa wa mfalme Ahasuero, Wayahudi walijiandaa vizuri kumshambulia mtu yeyote ambaye angejaribu kuwadhuru.

3. Ikawa viongozi wote wa mikoa, watawala, wakuu na maofisa wa mfalme pia waliwasaidia Wayahudi, maana wote walimwogopa Mordekai.

4. Mordekai sasa alikuwa mtu mwenye madaraka makubwa katika ikulu, na habari zake zilienea katika mikoa yote kwamba uwezo wake ulikuwa unazidi kuongezeka.

5. Basi, Wayahudi waliwashambulia maadui zao kwa upanga, wakawachinja, wakawaangamiza na kuwatenda kama walivyopenda.

6. Huko mjini Susa, Wayahudi waliwaua watu 500.

7. Pia waliwaua Parshandatha, Dalfoni, Aspatha,

8. Poratha, Adalia, Aridatha,

9. Parmashta, Arisai, Aridai na Waizatha,

10. wana kumi wa Hamani mwana wa Hamedatha, adui ya Wayahudi. Hata hivyo, hawakuteka nyara.

11. Siku hiyohiyo, mfalme alijulishwa idadi ya watu waliouawa katika mji mkuu wa Susa.

12. Ndipo mfalme akamwambia malkia Esta: “Katika mji mkuu peke yake Wayahudi wamewaua watu 500, pamoja na wana kumi wa Hamani. Unafikiri wamefanyaje huko mikoani! Unataka nini sasa? Maana utatimiziwa. Niambie, unataka nini zaidi, nawe utapewa.”

13. Esta akasema, “Ukiona ni vema, ewe mfalme, kesho waruhusu Wayahudi waliomo Susa wafanye kama agizo la leo lilivyokuwa. Tena, uamuru wana kumi wa Hamani watundikwe kwenye miti ya kuulia.”

14. Mfalme akaamuru hayo yatekelezwe, na tangazo likatolewa mjini Susa. Wana kumi wa Hamani wakanyongwa hadharani.

15. Siku ya kumi na nne ya mwezi wa Adari, Wayahudi walikusanyika tena, wakawaua watu 300 zaidi mjini Susa. Lakini hawakuteka nyara mali za watu.

16. Wayahudi waliokuwa katika mikoa nao pia walijiandaa kuyalinda maisha yao. Wakaokolewa kutoka kwa maadui wao; waliwaua watu wapatao 75,000, lakini hawakuchukua nyara.

Kusoma sura kamili Esta 9