Agano la Kale

Agano Jipya

Esta 1:7-17 Biblia Habari Njema (BHN)

7. Watu walipewa vinywaji katika vikombe mbalimbali vya dhahabu, naye mfalme alikuwa mkarimu sana wa divai ya kifalme.

8. Kila mtu alikunywa akashiba; mfalme alikuwa ametoa maagizo kwa watumishi wa ikulu wamhudumie kila mtu kadiri ya mahitaji yake.

9. Wakati huo huo, malkia Vashti naye aliwaandalia akina mama karamu ndani ya ikulu ya Ahasuero.

10. Siku ya saba ya karamu hiyo, mfalme Ahasuero, akiwa amejaa furaha kutokana na divai aliyokuwa amekunywa, aliwaita matowashi saba waliomhudumia yeye binafsi: Mehumani, Biztha, Harbona, Bigtha, Abagtha, Zethari na Karkasi.

11. Aliwaamuru hao wamlete kwake malkia Vashti, akiwa amevaa taji yake ya kimalkia. Malkia huyo alikuwa na sura ya kuvutia sana, hivyo mfalme alitaka kuwaonesha wageni wake na viongozi uzuri wake.

12. Lakini matowashi hao walipomweleza malkia amri ya mfalme, Vashti alikataa kutii. Jambo hilo lilimwudhi sana mfalme, akawa anawaka hasira moyoni.

13. Ilikuwa desturi ya mfalme kupata mawaidha kutoka kwa wenye hekima, hivyo aliwaita wanasheria na mahakimu ili wamshauri la kufanya.

14. Washauri wake wa kawaida walikuwa Karshena, Shethari, Admatha, Tarshishi, Maresi, Marsena na Memukani – viongozi saba wa Persia na Media waliokuwa na vyeo vya juu kabisa katika utawala wake.

15. Aliwauliza hivi: “Je, kulingana na sheria, afanyiwe nini malkia Vashti? Maana, nimewatuma matowashi wangu kwake, lakini yeye amekataa kuitii amri yangu, mimi mfalme Ahasuero!”

16. Hapo Memukani akamwambia mfalme na viongozi wake, “Licha ya kumkosea mfalme, malkia Vashti amewakosea viongozi na kila mtu katika mikoa ya mfalme Ahasuero!

17. Tendo hili la malkia Vashti litajulikana na wanawake wote, nao watawadharau waume zao, wakisema: ‘Mfalme Ahasuero aliamuru malkia Vashti aje kwake, lakini yeye akakataa.’

Kusoma sura kamili Esta 1