Agano la Kale

Agano Jipya

Danieli 5:15-23 Biblia Habari Njema (BHN)

15. Wenye hekima na wachawi walipoletwa hapa kusoma na kunieleza maana ya maandishi haya, walishindwa.

16. Lakini, nimesikia kwamba wewe unaweza kueleza vitendawili na kutambua mafumbo. Basi, kama ukifaulu kusoma maandishi haya na kunieleza maana yake, utavishwa mavazi rasmi ya zambarau na kuvishwa mkufu wa dhahabu shingoni mwako. Utapewa nafasi ya tatu katika ufalme huu.”

17. Danieli akamjibu mfalme Belshaza, “Waweza kukaa na zawadi zako ee mfalme au kumpa mtu mwingine. Hata hivyo, ee mfalme, nitakusomea maandishi hayo na kukueleza maana yake.

18. Ee mfalme, Mungu Mkuu alimpa baba yako mfalme Nebukadneza, ufalme, ukuu, fahari na utukufu.

19. Kwa sababu ya ukuu aliompa, watu wa makabila yote, mataifa yote na lugha zote walitetemeka na kumwogopa. Nebukadneza aliweza kumuua mtu yeyote aliyetaka na kumwacha hai yeyote aliyetaka. Aliyetaka kumpandisha cheo alimpandisha, aliyetaka kumshusha cheo alimshusha.

20. Lakini alipoanza kuwa na kiburi, akawa na roho ngumu na mwenye majivuno, aliondolewa katika kiti chake cha enzi, akanyanganywa utukufu wake.

21. Alifukuzwa mbali na wanaadamu, akili yake ikafanywa kama ya mnyama, akaishi na pundamwitu, akawa anakula majani kama ng'ombe. Alinyeshewa mvua mwilini mpaka alipotambua kwamba Mungu Mkuu ndiye atawalaye falme za wanaadamu, naye humweka mfalme yeyote amtakaye.

22. Lakini wewe Belshaza, mwanawe, ingawa unayajua haya yote, hukujinyenyekeza!

23. Badala yake umejikuza mwenyewe dhidi ya Bwana wa mbinguni: Umeleta vyombo vya nyumba yake Mungu ukavitumia kunywea divai, wewe, maofisa wako, wake zako na masuria wako, na kuisifu miungu iliyotengenezwa kwa fedha, dhahabu, shaba, chuma, miti na mawe; miungu ambayo haioni, haisikii wala haijui lolote. Lakini Mungu, ambaye uhai wako u mkononi mwake, na njia zako zi wazi mbele yake, hukumheshimu!

Kusoma sura kamili Danieli 5