Agano la Kale

Agano Jipya

Danieli 2:13-27 Biblia Habari Njema (BHN)

13. Basi, tangazo likaenea kuwa wenye hekima wote wauawe; Danieli na wenzake, nao pia wakatafutwa ili wauawe.

14. Basi, Danieli, kwa tahadhari na busara, alimwendea Arioko, mkuu wa kikosi cha walinzi wa mfalme na ambaye alipewa jukumu la kuwaua wenye hekima wa Babuloni,

15. akamwuliza, “Kwa nini amri ya mfalme ni kali hivyo?” Hapo Arioko akamsimulia Danieli kisa chote.

16. Ndipo Danieli alipomwendea mfalme na kumwomba ampe muda ili aweze kumjulisha mfalme maana ya ndoto yake.

17. Kisha, Danieli akarudi nyumbani, akawajulisha wenzake Hanania, Mishaeli na Azaria jambo hilo.

18. Aliwaambia wamwombe Mungu wa mbinguni awaonee huruma kuhusu fumbo hilo, ili wao wasiangamie pamoja na wenye hekima wengine wa Babuloni.

19. Ndipo Danieli alipofunuliwa fumbo hilo usiku katika maono. Naye Danieli akamshukuru Mungu wa mbinguni,

20. akasema,“Na litukuzwe milele na milele jina lake Mungu.Hekima na nguvu ni vyake.

21. Hubadilisha nyakati na majira,huwaondoa na kuwatawaza wafalme.Wenye busara huwapa hekima,wenye maarifa huwaongezea ufahamu.

22. Hufunua siri na mafumbo,ajua kilichoko gizani,mwanga wakaa kwake.

23. Kwako, ee Mungu wa wazee wangu,natoa shukrani na kukusifu,maana umenipa hekima na nguvu,umetujulisha kile tulichokuomba,umetujulisha kile kisa cha mfalme.”

24. Basi, Danieli akamwendea Arioko aliyekuwa ameteuliwa kuwaangamiza wenye hekima wa Babuloni, akamwambia, “Usiwaue wenye hekima wa Babuloni, ila nipeleke mimi mbele ya mfalme, nami nitamweleza maana ya ndoto yake.”

25. Basi, Arioko akampeleka Danieli mbele ya mfalme kwa haraka na kumwambia, “Nimempata mtu fulani miongoni mwa mateka wa Yuda anayeweza kukufasiria ndoto yako, ee mfalme.”

26. Mfalme akamwuliza Danieli, ambaye pia aliitwa Belteshaza, “Je, unaweza kunijulisha ndoto niliyoota na maana yake?”

27. Danieli akamjibu mfalme, “Hakuna wenye hekima, wachawi, waganga wala wanajimu wanaoweza kukujulisha fumbo hilo lako.

Kusoma sura kamili Danieli 2