Sura

  1. 1
  2. 2
  3. 3
  4. 4
  5. 5
  6. 6
  7. 7
  8. 8
  9. 9
  10. 10
  11. 11
  12. 12

Agano la Kale

Agano Jipya

Danieli 10 Biblia Habari Njema (BHN)

Maono ya Danieli kando ya mto Tigri

1. Mnamo mwaka wa tatu wa utawala wa mfalme Koreshi wa Persia, Danieli, aliyeitwa pia Belteshaza, alipewa ufunuo. Ufunuo huo ulikuwa wa kweli, lakini ulikuwa mgumu sana, haukueleweka. Hata hivyo alielewa ufunuo huo maana pia alifahamu maono.

2. “Wakati huo, mimi Danieli, nilikuwa nikiomboleza kwa muda wa majuma matatu.

3. Sikula chakula cha fahari, sikugusa nyama wala divai, na sikujipaka mafuta kwa muda wa majuma hayo yote matatu.

4. “Siku ya ishirini na nne ya mwezi wa kwanza, nilikuwa nimesimama kando ya mto Tigri.

5. Nikainua macho, nikamwona mtu amevaa mavazi ya kitani na kiunoni amejifunga mkanda wa dhahabu kutoka Ufazi.

6. Mwili wake ulingaa kama zabarajadi safi. Uso wake ulifanana na umeme, na macho yake yaliwaka kama miali ya moto. Miguu na mikono yake ilingaa kama shaba iliyosuguliwa sana. Sauti yake ilivuma kama sauti ya umati mkubwa wa watu.

7. “Mimi Danieli peke yangu niliona maono hayo. Wale watu waliokuwa pamoja nami hawakuyaona, lakini walishikwa na hofu sana, wakakimbia, wakajificha.

8. Hivyo, niliachwa peke yangu nikiangalia hayo maono ya kushangaza. Nguvu zikaniishia, na rangi yangu ikaharibika, nikabaki bila nguvu.

9. Nilipoisikia sauti yake, nilianguka chini kifudifudi, nikashikwa na usingizi mzito.

10. Hapo, mkono ukanigusa, ukanisimamisha, na kuimarisha miguu na mikono yangu.

11. Akaniambia, ‘Danieli, wewe unayependwa sana, simama wima usikilize kwa makini maneno nitakayosema, maana nimetumwa kwako.’ Alipokuwa akiniambia maneno haya, mimi nilisimama nikitetemeka.

12. Ndipo yeye akaniambia, ‘Danieli, usiogope. Mungu alilisikia ombi lako tangu siku ile ya kwanza ulipoamua kujinyenyekesha mbele yake ili upate ufahamu. Mimi nimekuja kwa ajili ya ombi lako hilo.

13. Mkuu wa ufalme wa Persia alinipinga kwa muda wa siku ishirini na moja. Lakini Mikaeli, mmoja wa wakuu, akaja kunisaidia, kwa hiyo nikamwacha huko pamoja na mkuu wa ufalme wa Persia,

14. nami nimekuja kukusaidia uyafahamu mambo yatakayowapata watu wako wakati ujao, kwani maono uliyoona yanahusu wakati ujao.’

15. “Alipokuwa ananiambia maneno hayo, niliangalia chini bila kuweza kuongea.

16. Kisha, mmoja mwenye umbo la binadamu, aliigusa midomo yangu, nami nilifungua midomo yangu na kumwambia huyo aliyesimama karibu nami, ‘Ee bwana, maono haya yameniletea maumivu makali hata nimeishiwa nguvu.

17. Mimi ni kama mtumwa mbele ya bwana wake. Nawezaje kuzungumza nawe? Sina nguvu na pumzi imeniishia!’

18. “Yule mmoja aliyeonekana kama mwanaadamu akanigusa kwa mara nyingine, akanitia nguvu.

19. Akaniambia, ‘Usiogope wewe unayependwa sana, uko salama. Uwe imara na hodari.’ Aliposema nami, nilipata nguvu, nikamwambia, ‘Bwana, umekwisha niimarisha; sema kile ulichotaka kusema.’

20. Naye akaniambia, ‘Je, unajua kwa nini nimekujia? Sasa ni lazima nirudi kupigana na malaika mlinzi wa Persia. Halafu, nitakapokuwa nimemshinda, malaika mlinzi wa mfalme wa Ugiriki atatokea.

21. Lakini nitakujulisha yale yaliyoandikwa katika kitabu cha ukweli. Sina mwingine wa kunisaidia kuwashinda hawa isipokuwa Mikaeli, malaika mlinzi wenu.