Agano la Kale

Agano Jipya

2 Wafalme 9:2-16 Biblia Habari Njema (BHN)

2. na utakapofika huko, mtafute Yehu mwana wa Yehoshafati na mjukuu wa Nimshi. Mchukue kando chumbani mbali na wenzake,

3. kisha chukua chupa hii ya mafuta, ummiminie kichwani na kumwambia, ‘Mwenyezi-Mungu asema hivi: Nimekupaka mafuta kuwa mfalme wa Israeli.’ Kisha fungua mlango na kuondoka upesi utakavyoweza.”

4. Basi, Nabii huyo kijana akaenda Ramothi Gileadi.

5. Alipofika aliwakuta makamanda wa jeshi mkutanoni. Akasema “Nina ujumbe wako, kamanda.”Yehu akamwuliza, “Ni nani kati yetu unayemwambia?” Akamjibu, “Wewe, kamanda.”

6. Ndipo wote wawili wakaingia chumba cha ndani na huko nabii akamtia Yehu mafuta kichwani na kumwambia, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, asema, ‘Nakupaka mafuta uwe mfalme juu ya watu wangu Israeli.

7. Nawe utaipiga jamaa ya bwana wako Ahabu ili nimlipize kisasi Yezebeli damu ya watumishi wangu manabii na ya watumishi wangu wote.

8. Utafanya hivyo kwa sababu jamaa yote ya Ahabu itaangamia; pia nitamkatilia mbali kila mwanamume wa jamaa ya Ahabu awe mtumwa au mtu huru.

9. Jamaa yake itakuwa kama jamaa ya Yeroboamu mwana wa Nebati na ya Baasha mwana wa Ahiya.

10. Yezebeli hatazikwa na mtu, maiti yake italiwa na mbwa katika nchi ya Yezreeli.’” Baada ya kusema hayo, nabii akaondoka chumbani na kukimbia.

11. Yehu aliporudi kwa wenzake, mmoja wao alimwuliza, “Kuna shida yoyote? Mwendawazimu huyu alitaka nini kwako?” Yehu akawajibu, “Mnajua alichotaka.”

12. Nao wakamwambia, “Hiyo si kweli! Tuambie alilosema!” Akawaambia, “Aliniambia kwamba Mwenyezi-Mungu amesema, ‘Nimekutawaza kuwa mfalme wa Israeli.’”

13. Mara moja makamanda wenzake wakavua mavazi yao, wakayarundika pamoja kwenye ngazi ili asimame juu yake, wakapiga tarumbeta na kupaza sauti, “Yehu ni mfalme!”

14. Yehu mwana wa Yehoshafati, ambaye pia alikuwa mjukuu wa Nimshi, alikula njama dhidi ya Yoramu. Yoramu na watu wote wa Israeli walikuwa Ramoth-gileadi kulinda zamu dhidi ya mfalme Hazaeli wa Aramu.

15. Lakini mfalme Yoramu alikuwa amerudi Yezreeli ili apone majeraha aliyopata wakati wa kupigana vitani na mfalme Hazaeli wa Aramu. Yehu aliwaambia maofisa wenzake; “Ikiwa mtakubaliana nami, mtu yeyote asitoke Ramothi kwenda Yezreeli kupeleka habari hizi.”

16. Ndipo akapanda gari lake na kuelekea Yezreeli. Yoramu alikuwa bado hajapona, na Ahazia mfalme wa Yuda alikuwa amemtembelea.

Kusoma sura kamili 2 Wafalme 9