Agano la Kale

Agano Jipya

2 Wafalme 6:13-24 Biblia Habari Njema (BHN)

13. Mfalme akawaambia, “Nendeni mkapeleleze mjue mahali alipo nami nitawatuma watu wamkamate.” Basi, wakamwarifu kwamba Elisha alikuwa huko Dothani.

14. Kwa hiyo mfalme akapeleka huko jeshi kubwa pamoja na farasi na magari ya kukokotwa. Jeshi hilo likafika huko wakati wa usiku na kuuzingira mji.

15. Mtumishi wa Elisha alipoamka mapema kesho yake na kutoka nje, akaona jeshi pamoja na farasi na magari ya kukokotwa limeuzingira mji. Akarudi ndani akasema, “Ole wetu, ee, Bwana wangu! Sasa tutafanya nini?”

16. Elisha akamjibu, “Usiogope kwa sababu walio pamoja nasi ni wengi kuliko walio pamoja nao.”

17. Kisha Elisha akaomba, “Ee Mwenyezi-Mungu, umfumbue macho ili apate kuona!” Basi, Mwenyezi-Mungu akamfumbua macho huyo kijana, akaona farasi na magari ya moto yakiwa kila mahali katika mlima wote, kumzunguka Elisha.

18. Waaramu waliposhambulia, Elisha alimwomba Mwenyezi-Mungu akisema, “Nakuomba uwafanye watu hawa wawe vipofu!” Mwenyezi-Mungu akasikiliza ombi lake na kuwafanya vipofu.

19. Ndipo Elisha akawaendea na kuwaambia, “Mmepotea njia. Huu siyo mji ambao mnautafuta. Nifuateni nami nitawapeleka kwa yule mnayemtafuta.” Naye akawaongoza mpaka Samaria.

20. Mara walipoingia mjini, Elisha akaomba, akisema, “Ee Mwenyezi-Mungu, wafumbue macho ili waone.” Mwenyezi-Mungu akasikia ombi lake, akawafumbua macho. Nao wakajikuta wako katikati ya mji wa Samaria.

21. Mfalme wa Israeli alipowaona Waaramu, alimwuliza Elisha, “Je, baba, niwaue?”

22. Elisha akajibu, “La, usiwaue. Kwani hawa unaotaka kuwaua uliwateka kwa upanga wako na mshale wako? Wape chakula na maji, wale na kunywa kisha uwaache warudi kwa bwana wao.”

23. Mfalme wa Israeli akawafanyia karamu kubwa; walipomaliza kula na kunywa, akawarudisha kwa bwana wao. Toka wakati huo, Waaramu hawakuishambulia tena nchi ya Israeli.

24. Baadaye, mfalme Ben-hadadi wa Aramu akakusanya jeshi lake lote akatoka na kuuzingira mji wa Samaria.

Kusoma sura kamili 2 Wafalme 6