Agano la Kale

Agano Jipya

2 Wafalme 4:28-43 Biblia Habari Njema (BHN)

28. Huyo mama akamwambia, “Bwana wangu, je, si nilikuomba mtoto? Kwani sikukusihi usije ukanipa matumaini ambayo yangenipa huzuni baadaye?”

29. Elisha akamwambia Gehazi, “Chukua fimbo yangu, uondoke mara moja. Usisimame njiani kumwamkia mtu yeyote, na mtu yeyote akikuamkia njiani, usipoteze wakati kurudisha salamu. Nenda moja kwa moja mpaka nyumbani na kuweka fimbo yangu juu ya mtoto.”

30. Mwanamke akamwambia Elisha, “Kama Mwenyezi-Mungu aishivyo na kama wewe uishivyo, sitakuacha.” Basi Elisha akaondoka na kufuatana naye.

31. Gehazi akatangulia mbele, na alipofika akaweka fimbo ya Elisha juu ya uso wa mtoto, lakini hakukuonekana dalili yoyote ya uhai. Akarudi na kukutana na Elisha, akamwambia, “Kijana hakufufuka.”

32. Elisha alipofika, akaingia peke yake chumbani na kuona maiti ya kijana kitandani.

33. Basi, akafunga mlango na kumwomba Mwenyezi-Mungu.

34. Ndipo akajilaza juu ya mtoto, mdomo wake juu ya mdomo wa mtoto, na macho yake juu ya macho ya mtoto na mikono yake juu ya mikono ya mtoto. Na alipokuwa amekaa hivyo, mwili wa mtoto ukaanza kupata joto.

35. Elisha akasimama na kutembeatembea chumbani, kisha akarudi na kujilaza tena juu ya mtoto. Mtoto akapiga chafya mara saba, halafu akafungua macho.

36. Elisha akamwita Gehazi na kumwambia, “Mwite yule Mshunami.” Alipoitwa Elisha akamwambia, “Mchukue mwanao.”

37. Akainama miguuni pa Elisha kwa shukrani na kumchukua mwanawe.

38. Elisha akarudi Gilgali wakati nchini kulikuwa na njaa. Siku moja, alipokuwa akifundisha wanafunzi wa manabii alimwambia mtumishi wake, “Weka chungu kikubwa motoni, uwapikie manabii.”

39. Mmoja wao akaenda shambani na kuchuma mboga. Huko akaona mtango-mwitu, akachuma matango mengi kadiri alivyoweza kuchukua. Akaja nayo, akayakatakata na kuyatia chunguni bila kuyajua.

40. Chakula kikapakuliwa. Lakini walipokionja wakamlilia Elisha wakisema, “Ee mtu wa Mungu, chakula hiki kitatuua!” Nao hawakuweza kukila.

41. Elisha akaagiza aletewe unga. Akaletewa unga, naye akautia ndani ya chungu na kusema, “Sasa wape chakula wale.” Wakakila, na hapo hakikuwadhuru.

42. Mtu Mmoja akatoka Baal-shalisha, akamletea Elisha mikate ishirini iliyotengenezwa kwa shayiri ya malimbuko ya mavuno ya mwaka huo na masuke mabichi ya ngano guniani. Elisha akamwagiza Gehazi awape watu wale.

43. Mtumishi wake akasema, “Sitawapa kwa sababu hakitawatosha watu 100”. Elisha akasema, “Wape wale, kwa sababu Mwenyezi-Mungu amesema kwamba watakula washibe na kingine kitabaki.”

Kusoma sura kamili 2 Wafalme 4