Agano la Kale

Agano Jipya

2 Wafalme 3:19-27 Biblia Habari Njema (BHN)

19. Mtashinda kila mji wenye ngome na kila mji mzuri; mtaikata miti yao yote, mtaziba chemchemi zote za maji, na kuyaharibu mashamba yao yote yenye rutuba kwa kuyajaza mawe.”

20. Kesho yake asubuhi, wakati wa kutambikia, maji yakatiririka kutoka upande wa Edomu na kujaa kila mahali bondeni.

21. Wamoabu walipopata habari kwamba hao wafalme watatu wamekuja kuwashambulia, watu wote wawezao kuvaa silaha kuanzia vijana mpaka wazee, waliitwa, wakapewa silaha na kuwekwa mpakani tayari kwa vita.

22. Walipoamka asubuhi iliyofuata, jua lilikuwa linametameta juu ya maji hayo; walipoyatazama yakaonekana kuwa mekundu kama damu.

23. Wakasema, “Hii ni damu! Bila shaka hawa wafalme watatu wamepigana wao kwa wao na kuuana! Twendeni tukachukue nyara!”

24. Lakini walipofika katika kambi ya Israeli, watu wa Israeli waliwashambulia, nao wakakimbia mbele yao. Watu wa Israeli wakawafuatia mpaka Moabu huku wakiwaua

25. na kuibomoa miji yao. Kila walipopita penye shamba zuri, kila mtu alilirushia jiwe mpaka kila shamba likajaa mawe; kadhalika wakaziziba chemchemi zote za maji na kukata miti yote mizuri. Hatimaye, ukabaki mji mkuu wa Kir-haresethi peke yake, ambao pia wapiga kombeo waliuzingira na kuuteka.

26. Mfalme wa Moabu alipoona kwamba vita vinamwendea vibaya, alichukua watu wake 700 wenye kupigana kwa mapanga, akikusudia kupenya majeshi ya adui zake mkabala na mfalme wa Edomu, lakini hakufaulu.

27. Hapo akamchukua mwanawe wa kwanza ambaye angekuwa mfalme mahali pake, akamtoa kuwa sadaka ya kuteketezwa juu ya ukuta wa mji. Watu wa Israeli walipoona hayo, wakachukizwa mno. Wakauacha mji huo na kurudi nchini kwao.

Kusoma sura kamili 2 Wafalme 3