Agano la Kale

Agano Jipya

2 Wafalme 23:24-33 Biblia Habari Njema (BHN)

24. Tena, ili mfalme Yosia atekeleze sheria zote zilizoandikwa katika kitabu alichokipata kuhani mkuu Hilkia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, aliondoa katika nchi ya Yuda na Yerusalemu, wachawi, watabiri, vinyago vya miungu, sanamu za miungu pamoja na vitu vyote vya kuchukiza.

25. Kabla ya Yosia au baada yake hakuna mfalme yeyote aliyekuwa kama yeye, ambaye alimtumikia Mwenyezi-Mungu kwa moyo wake wote, kwa nguvu zake zote na kwa roho yake yote kulingana na sheria ya Mose.

26. Hata hivyo, Mwenyezi-Mungu hakuacha ukali wa ghadhabu yake nyingi, kwa sababu hasira yake iliwaka dhidi ya Yuda kwa ajili ya vitendo vya kukasirisha, ambavyo Manase alifanya dhidi yake.

27. Naye Mwenyezi-Mungu alisema, “Nitawafukuza watu wa Yuda kutoka mbele yangu kama vile nilivyofanya kwa watu wa Israeli; nitaukataa mji wa Yerusalemu ambao niliuchagua niliposema, ‘Jina langu litakuwa humo.’”

28. Matendo mengine ya Yosia na yale yote aliyofanya yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Yuda.

29. Wakati wa kutawala kwake, Farao Neko wa Misri alikwenda mpaka mto Eufrate ili kukutana na mfalme wa Ashuru. Naye mfalme Yosia akaondoka ili kupambana naye; lakini Farao Neko alipomwona alimuua kule Megido.

30. Maofisa wake wakaibeba maiti yake katika gari na kuirejesha Yerusalemu walikomzika katika kaburi lake mwenyewe. Kisha watu wa Yuda wakamchukua Yehoahazi mwana wa Yosia wakampaka mafuta na kumtawaza kuwa mfalme mahali pa baba yake.

31. Yehoahazi alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitatu alipoanza kutawala, akatawala kwa miezi mitatu huko Yerusalemu. Mama yake alikuwa Hamutali binti Yeremia wa Libna.

32. Yehoahazi alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu kama babu zake walivyofanya.

33. Ili asiendelee kutawala huko Yerusalemu, Farao Neko alimtia nguvuni huko Ribla katika nchi ya Hamathi, akaitoza nchi kodi ya kilo 3,400 za madini ya fedha na kilo 34 za dhahabu.

Kusoma sura kamili 2 Wafalme 23