Agano la Kale

Agano Jipya

2 Wafalme 10:27-36 Biblia Habari Njema (BHN)

27. Wakaharibu nguzo pamoja na hekalu; wakaligeuza hekalu kuwa choo; na hivyo ndivyo ilivyo mpaka hivi leo.

28. Hivyo ndivyo Yehu alivyofuta ibada za Baali katika Israeli.

29. Lakini alifuata dhambi ya Yeroboamu mwana wa Nebati ya kuwaongoza Waisraeli watende dhambi. Aliweka sanamu za ndama wa dhahabu huko Betheli na Dani.

30. Mwenyezi-Mungu akamwambia Yehu, “Umewatendea wazawa wa Ahabu yale yote niliyotaka uwatendee. Kwa hiyo nimekuahidi kuwa wazawa wako hadi kizazi cha nne watatawala Israeli.”

31. Lakini Yehu hakutii sheria za Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kwa moyo wake wote. Badala yake, alifuata mfano wa Yeroboamu aliyewapotosha watu wa Israeli wakatenda dhambi.

32. Wakati huo Mwenyezi-Mungu alianza kupunguza eneo la nchi ya Israeli. Mfalme Hazaeli wa Aramu akashinda nchi yote ya Israeli,

33. kutoka upande wa mashariki ya mto Yordani, na nchi za Gileadi, Gadi, Reubeni na Manase na kutoka Aroeri ulioko kwenye bonde la Arnoni, kwenye nchi za Gileadi na Bashani.

34. Matendo mengine yote ya Yehu na vitendo vyake vya ushujaa yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Israeli.

35. Akafariki na kuzikwa Samaria. Mwanae Yehoahazi akatawala mahali pake.

36. Yehu alitawala Israeli akiwa Samaria kwa miaka ishirini na minane.

Kusoma sura kamili 2 Wafalme 10