Agano la Kale

Agano Jipya

2 Wafalme 1:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Baada ya kifo cha Ahabu, watu wa Moabu waliasi wasitawaliwe na Israeli.

2. Mfalme Ahazia alipokuwa Samaria alianguka kutoka chumba kilichokuwa paani mwa nyumba yake, akaumia vibaya. Kwa hiyo akawatuma wajumbe, akawaambia, “Nendeni kwa Baal-zebubu, mungu wa mji wa Ekroni, mkamwulize kama nitapona ugonjwa huu.”

3. Lakini malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwambia nabii Elia kutoka Tishbe, aende kukutana na wajumbe hao na kuwauliza, “Kwa nini mnakwenda kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni? Je, hakuna Mungu nchini Israeli?

4. Mwambieni mfalme kwamba Mwenyezi-Mungu amesema hivi: ‘Hutashuka katika kitanda ulichokipanda; hakika utakufa!’”

5. Basi, Elia akawaendea. Wale wajumbe wakarudi kwa mfalme, naye akawauliza, “Mbona mmerudi?”

6. Wakamjibu, “Tumekutana na mtu ambaye alitutuma turudi kukuambia kwamba Mwenyezi-Mungu amesema hivi: ‘Kwa nini unatuma wajumbe kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni? Je, hakuna Mungu nchini Israeli? Hutashuka katika kitanda ulichokipanda; bali hakika utakufa!’”

7. Mfalme akauliza, “Ni mtu gani huyo aliyekutana nanyi na kuwaambieni mambo hayo?”

8. Wao wakamjibu, “Alikuwa amevaa vazi la manyoya na mshipi wa ngozi kiunoni.” Mfalme akasema, “Huyo ni Elia kutoka Tishbe!”

Kusoma sura kamili 2 Wafalme 1