Agano la Kale

Agano Jipya

2 Samueli 7:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Wakati mfalme Daudi alipokuwa akikaa katika ikulu, naye Mwenyezi-Mungu amemuwezesha kuwa na amani na adui zake kila upande,

2. mfalme Daudi akamwambia nabii Nathani, “Hebu tazama; mimi ninakaa katika nyumba iliyojengwa kwa mierezi, lakini sanduku la Mungu linakaa hemani.”

3. Nathani akamwambia mfalme, “Nenda ufanye chochote unachofikiria moyoni mwako, kwa kuwa Mwenyezi-Mungu yu pamoja nawe.”

4. Lakini usiku uleule neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Nathani,

5. “Nenda ukamwambie mtumishi wangu Daudi, ‘Mwenyezi-Mungu asema hivi: Je, wewe utanijengea nyumba ya kukaa?

6. Tangu siku ile nilipowatoa Waisraeli nchini Misri mpaka hivi leo sijaishi kwenye nyumba. Nimetembea kila mahali nikiwa ninakaa hemani.

7. Je, kila mahali ambako nimekwenda na Waisraeli wote nimemwuliza mtu yeyote wa Israeli ambaye nilimwamuru awachunge watu wa Israeli: Kwa nini hajanijengea nyumba ya mierezi?

8. Kwa hiyo basi, mwambie mtumishi wangu Daudi: Mwenyezi-Mungu wa majeshi anasema hivi: Nilikutoa malishoni ulikokuwa unawachunga kondoo, ili uwe mkuu wa watu wangu Israeli.

9. Tangu wakati huo nimekuwa pamoja nawe kokote ulikokwenda na nimewaangamiza adui zako wote mbele yako. Nitakufanya kuwa maarufu kama wakuu wengine duniani.

10. Nami nitawachagulia watu wangu wa Israeli mahali pa kuishi, niwapandikize, ili waishi mahali pao wenyewe, wasisumbuliwe tena. Nao watu wakatili wanaotumia nguvu hawatawatesa tena kama hapo awali,

11. tangu wakati nilipowateua waamuzi juu ya watu wangu Israeli, nami nitakulinda kutokana na adui zako wote. Zaidi ya yote, mimi Mwenyezi-Mungu nakutangazia kuwa nitakujengea nyumba.

Kusoma sura kamili 2 Samueli 7