Agano la Kale

Agano Jipya

2 Samueli 6:7-17 Biblia Habari Njema (BHN)

7. Hapo, hasira ya Mwenyezi-Mungu ikawaka dhidi ya Uza. Mungu akamuua palepale. Uza akafa papo hapo kando ya sanduku la Mungu.

8. Naye Daudi alikasirika kwa kuwa Mwenyezi-Mungu alimwadhibu Uza kwa hasira. Hivyo, mahali hapo pakaitwa Peres-uza mpaka hivi leo.

9. Siku hiyo Daudi alimwogopa Mwenyezi-Mungu akasema, “Sasa litanijiaje sanduku la Mwenyezi-Mungu?”

10. Kwa hiyo, Daudi hakuwa tayari kulipeleka sanduku la Mwenyezi-Mungu ndani ya mji wa Daudi, bali Daudi alilipeleka nyumbani kwa Obed-edomu, Mgiti.

11. Sanduku hilo la Mwenyezi-Mungu lilikaa nyumbani kwa Obed-edomu kwa muda wa miezi mitatu; naye Mwenyezi-Mungu akambariki Obed-edomu pamoja na jamaa yake.

12. Mfalme Daudi aliposikia kuwa Mwenyezi-Mungu ameibariki jamaa ya Obed-edomu na vitu vyote alivyokuwa navyo kwa sababu ya sanduku la Mungu, akaenda kulichukua sanduku la agano kutoka nyumbani kwa Obed-edomu na kulipeleka kwenye mji wa Daudi kwa shangwe.

13. Watu wale waliolibeba sanduku la Mwenyezi-Mungu kila walipopiga hatua sita, Daudi alitoa tambiko: Fahali na ndama mmoja mnono.

14. Daudi akiwa amejifunga kizibao cha kuhani kiunoni mwake alicheza kwa nguvu zake zote mbele ya Mwenyezi-Mungu.

15. Hivyo, yeye na Waisraeli wote walilipeleka sanduku la Mwenyezi-Mungu hadi mjini mwa Daudi kwa shangwe na sauti kubwa ya tarumbeta.

16. Sanduku la Mwenyezi-Mungu lilipokuwa linaingia katika mji wa Daudi, Mikali binti Shauli alichungulia dirishani akamwona mfalme Daudi akirukaruka na kucheza mbele ya Mwenyezi-Mungu; basi, akamdharau moyoni mwake.

17. Kisha waliliingiza sanduku la Mwenyezi-Mungu ndani ya hema ambalo Daudi alikuwa amelipiga hapo na kuliweka mahali pake. Naye Daudi akatoa tambiko za kuteketezwa na tambiko za amani mbele ya Mwenyezi-Mungu.

Kusoma sura kamili 2 Samueli 6