Agano la Kale

Agano Jipya

2 Samueli 6:5-16 Biblia Habari Njema (BHN)

5. Daudi na watu wote wa Israeli, wakawa wanaimba nyimbo na kucheza kwa nguvu zao zote, mbele ya Mwenyezi-Mungu. Walipiga ala za muziki zilizotengenezwa kwa mvinje: Vinubi, vinanda, matari, kayamba na matoazi.

6. Walipofika kwenye uwanja wa kupuria nafaka wa Nakoni, Uza aliunyosha mkono wake na kulishika sanduku la Mungu kwa sababu wale ng'ombe walijikwaa.

7. Hapo, hasira ya Mwenyezi-Mungu ikawaka dhidi ya Uza. Mungu akamuua palepale. Uza akafa papo hapo kando ya sanduku la Mungu.

8. Naye Daudi alikasirika kwa kuwa Mwenyezi-Mungu alimwadhibu Uza kwa hasira. Hivyo, mahali hapo pakaitwa Peres-uza mpaka hivi leo.

9. Siku hiyo Daudi alimwogopa Mwenyezi-Mungu akasema, “Sasa litanijiaje sanduku la Mwenyezi-Mungu?”

10. Kwa hiyo, Daudi hakuwa tayari kulipeleka sanduku la Mwenyezi-Mungu ndani ya mji wa Daudi, bali Daudi alilipeleka nyumbani kwa Obed-edomu, Mgiti.

11. Sanduku hilo la Mwenyezi-Mungu lilikaa nyumbani kwa Obed-edomu kwa muda wa miezi mitatu; naye Mwenyezi-Mungu akambariki Obed-edomu pamoja na jamaa yake.

12. Mfalme Daudi aliposikia kuwa Mwenyezi-Mungu ameibariki jamaa ya Obed-edomu na vitu vyote alivyokuwa navyo kwa sababu ya sanduku la Mungu, akaenda kulichukua sanduku la agano kutoka nyumbani kwa Obed-edomu na kulipeleka kwenye mji wa Daudi kwa shangwe.

13. Watu wale waliolibeba sanduku la Mwenyezi-Mungu kila walipopiga hatua sita, Daudi alitoa tambiko: Fahali na ndama mmoja mnono.

14. Daudi akiwa amejifunga kizibao cha kuhani kiunoni mwake alicheza kwa nguvu zake zote mbele ya Mwenyezi-Mungu.

15. Hivyo, yeye na Waisraeli wote walilipeleka sanduku la Mwenyezi-Mungu hadi mjini mwa Daudi kwa shangwe na sauti kubwa ya tarumbeta.

16. Sanduku la Mwenyezi-Mungu lilipokuwa linaingia katika mji wa Daudi, Mikali binti Shauli alichungulia dirishani akamwona mfalme Daudi akirukaruka na kucheza mbele ya Mwenyezi-Mungu; basi, akamdharau moyoni mwake.

Kusoma sura kamili 2 Samueli 6