Agano la Kale

Agano Jipya

2 Samueli 6:13-22 Biblia Habari Njema (BHN)

13. Watu wale waliolibeba sanduku la Mwenyezi-Mungu kila walipopiga hatua sita, Daudi alitoa tambiko: Fahali na ndama mmoja mnono.

14. Daudi akiwa amejifunga kizibao cha kuhani kiunoni mwake alicheza kwa nguvu zake zote mbele ya Mwenyezi-Mungu.

15. Hivyo, yeye na Waisraeli wote walilipeleka sanduku la Mwenyezi-Mungu hadi mjini mwa Daudi kwa shangwe na sauti kubwa ya tarumbeta.

16. Sanduku la Mwenyezi-Mungu lilipokuwa linaingia katika mji wa Daudi, Mikali binti Shauli alichungulia dirishani akamwona mfalme Daudi akirukaruka na kucheza mbele ya Mwenyezi-Mungu; basi, akamdharau moyoni mwake.

17. Kisha waliliingiza sanduku la Mwenyezi-Mungu ndani ya hema ambalo Daudi alikuwa amelipiga hapo na kuliweka mahali pake. Naye Daudi akatoa tambiko za kuteketezwa na tambiko za amani mbele ya Mwenyezi-Mungu.

18. Daudi alipomaliza kutoa tambiko za kuteketezwa na za amani, aliwabariki watu kwa jina la Mwenyezi-Mungu wa majeshi,

19. na akawagawia watu wote, kundi lote la Waisraeli, wanaume na wanawake, kila mmoja, mkate, kipande cha nyama na mkate wa zabibu. Baadaye, watu wote waliondoka, kila mtu akarudi nyumbani kwake.

20. Daudi aliporudi nyumbani kwake ili kuibariki jamaa yake, Mikali, binti Shauli, alikwenda kumlaki, akasema, “Ajabu ya mfalme wa Israeli kujiheshimu leo, kwa kujifunua uchi wake mbele ya watumishi wake wa kiume na wa kike kama mshenzi avuavyo mavazi yake mbele ya watu bila aibu!”

21. Daudi akamwambia Mikali, “Nilikuwa mbele ya Mwenyezi-Mungu ambaye alinichagua mimi badala ya baba yako, na jamaa yake, ili kuniteua kuwa mkuu juu ya Israeli, watu wake Mwenyezi-Mungu, kwa hiyo mimi nitacheza tu mbele ya Mwenyezi-Mungu.

22. Nitajishusha mwenyewe zaidi kuliko sasa. Wewe utaniona kuwa si kitu, lakini hao watumishi wa kike uliowasema wataniheshimu.”

Kusoma sura kamili 2 Samueli 6