Agano la Kale

Agano Jipya

2 Samueli 3:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Kulikuwa na vita vya muda mrefu kati ya watu walioiunga mkono jamaa ya Shauli, na wale walioiunga mkono jamaa ya Daudi. Lakini Daudi alizidi kupata nguvu zaidi na zaidi, ambapo upande wa Shauli ulizidi kudhoofika zaidi na zaidi.

2. Watoto wa kiume aliozaliwa Daudi huko Hebroni walikuwa: Amnoni, mzaliwa wake wa kwanza, mama yake alikuwa Ahinoamu kutoka Yezreeli;

3. Kileabu, mzaliwa wake wa pili, mama yake alikuwa Abigaili, mjane wa Nabali kutoka Karmeli; Absalomu, mzaliwa wake wa tatu, mama yake alikuwa Maaka, bintiye Talmai mfalme wa Geshuri;

4. Adoniya, mzaliwa wake wa nne, mama yake alikuwa Hagithi; Shefatia, mzaliwa wake wa tano, mama yake alikuwa Abitali,

5. na Ithreamu, mzaliwa wake wa sita, mama yake alikuwa Egla, mke wake Daudi. Daudi alizaliwa wana hawa wote alipokuwa huko Hebroni.

6. Kadiri vita vilivyoendelea kati ya jamaa ya Daudi na ile ya Shauli, Abneri alizidi kujiimarisha katika jamaa ya Shauli.

7. Shauli alikuwa na suria mmoja aitwaye Rispa, binti Aya. Basi, wakati mmoja, Ishboshethi akamwuliza Abneri, “Kwa nini umelala na suria wa baba yangu?”

8. Abneri alikasirika sana kutokana na maneno ya Ishboshethi, akasema: “Je, unafikiri mimi naweza kumsaliti Shauli? Je, unafikiri kuwa mimi naitumikia jamaa ya Yuda? Tazama, mimi nimekuwa mtiifu kwa jamaa ya baba yako Shauli, ndugu zake, rafiki zake na sijakutia mikononi mwa Daudi hadi leo. Hata hivyo, leo hii unaniona kuwa mwenye hatia kwa ajili ya mwanamke.

9. Mungu aniue ikiwa sitatekeleza yote ambayo Mwenyezi-Mungu alimwapia Daudi.

10. Mwenyezi-Mungu alimwapia Daudi kuwa atauhamisha ufalme kutoka jamaa ya Shauli na kumpa yeye. Naye atatawala Israeli na Yuda kutoka Dani hadi Beer-sheba.”

11. Ishboshethi hakuweza kusema neno, kwa kuwa alikuwa anamwogopa Abneri.

12. Basi, Abneri akatuma wajumbe kwa Daudi, huko Hebroni wakamwambie, “Je, nchi hii ni mali ya nani? Fanya agano na mimi, nami nitakusaidia kuifanya Israeli yote iwe chini yako.”

13. Daudi akamjibu, “Vema, nitafanya agano nawe. Lakini ninakutaka jambo moja kwamba kabla hujaniona sharti kwanza uniletee Mikali binti wa Shauli. Hapo utaniona.”

14. Daudi pia alituma wajumbe kwa Ishboshethi mwana wa Shauli akisema, “Nirudishie mke wangu Mikali ambaye nilimwoa kwa magovi 100 ya Wafilisti.”

Kusoma sura kamili 2 Samueli 3