Agano la Kale

Agano Jipya

2 Samueli 19:30-41 Biblia Habari Njema (BHN)

30. Lakini Mefiboshethi akamwambia mfalme, “Mruhusu Siba aichukue nchi yote peke yake. Mimi nimetosheka kwamba wewe bwana wangu mfalme umerudi nyumbani salama.”

31. Barzilai Mgileadi alikuwa amefika kutoka Rogelimu. Alikuwa amekwenda pamoja na mfalme kwenye mto Yordani ili kumsindikiza hadi ngambo ya mto.

32. Barzilai alikuwa mzee sana, mwenye umri wa miaka themanini. Naye Barzilai alikuwa amemtunza mfalme alipokaa huko Mahanaimu, kwa kuwa alikuwa tajiri sana.

33. Basi, mfalme Daudi akamwambia Barzilai, “Twende wote huko Yerusalemu nami nitakutunza.”

34. Lakini Barzilai akamwambia mfalme, “Je, nina miaka mingi ya kuishi ndipo niende nawe mfalme mpaka Yerusalemu?

35. Mimi leo nina umri wa miaka themanini. Je, nina uwezo wa kubainisha yaliyo mazuri na yale yasiyo mazuri? Je, mimi mtumishi wako, naweza kutambua ladha ya kile ninachokula au kunywa? Je, nitaweza kutambua uzuri wa sauti za waimbaji wanaume au wanawake? Kwa nini mimi mtumishi wako niwe mzigo wa ziada kwako, bwana wangu mfalme?

36. Mimi mtumishi wako nitakwenda nawe mwendo mfupi ngambo ya Yordani. Kwa nini, mfalme anilipe zawadi kubwa hivyo?

37. Nakuomba, uniruhusu mimi mtumishi wako, nifie katika mji wangu, karibu na kaburi la baba yangu na mama yangu. Lakini huyu mtumishi wako Kimhamu, mruhusu aende pamoja nawe bwana wangu mfalme, na mtendee yeye lolote unaloona ni jema.”

38. Mfalme akamwambia, “Kimhamu atakwenda nami, na nitamtendea lolote lililo jema kwako. Na lolote utakalotaka nikutendee, nitakutendea.”

39. Ndipo watu wote wakavuka mtoni Yordani na mfalme naye akavuka. Mfalme akambusu na kumbariki Barzilai, na Barzilai akarudi nyumbani kwake.

40. Mfalme aliendelea mpaka Gileadi, Kimhamu akawa anafuatana naye. Watu wote wa Yuda na nusu ya watu wa Israeli walikuwa wakimsindikiza mfalme.

41. Kisha, watu wote wa Israeli wakaja kwa mfalme na kumwambia, “Kwa nini ndugu zetu watu wa Yuda walikuwa wamekuiba ukiwa njiani, wakakuvusha mto Yordani, wewe na jamaa yako, pamoja na watu wako?”

Kusoma sura kamili 2 Samueli 19