Agano la Kale

Agano Jipya

2 Samueli 18:3-14 Biblia Habari Njema (BHN)

3. Lakini watu wakamwambia, “Hutatoka. Maana, ikiwa tutakimbia, hawatajali juu yetu. Ikiwa nusu yetu watakufa, pia hawatajishughulisha juu yetu. Lakini wewe una thamani kuliko watu 10,000 miongoni mwetu. Hivyo inafaa wewe ubaki mjini na kutupelekea msaada ukiwa mjini.”

4. Mfalme akawaambia, “Lolote mnaloona ni bora kwenu, nitalitenda.” Hivyo, mfalme akasimama kando ya lango, huku jeshi lake likipita: Mamia na maelfu.

5. Mfalme akawaamuru Yoabu, Abishai na Itai, “Kwa ajili yangu, mtendeeni yule kijana Absalomu kwa upole.” Watu wote walimsikia mfalme alipoamuru makamanda wake kuhusu Absalomu.

6. Hivyo, jeshi la Daudi likaenda nyikani kupigana na watu wa Israeli. Mapigano hayo yalifanyika katika msitu wa Efraimu.

7. Watumishi wa Daudi waliwashinda watu wa Israeli. Mauaji ya siku hiyo yalikuwa makubwa kwani watu 20,000 waliuawa.

8. Mapigano hayo yalienea nchini kote na watu wengi walikufa msituni kuliko wale waliouawa kwa upanga vitani.

9. Kisha Absalomu, akiwa amepanda nyumbu, alikutana na watumishi wa Daudi. Nyumbu huyo alipokuwa anapita chini ya tawi kubwa la mwaloni, hapo kichwa cha Absalomu kikakwama kwenye mwaloni. Absalomu akaachwa ananinginia juu. Lakini nyumbu wake akaendelea mbele.

10. Mtu fulani aliyeona tukio hilo, akamwambia Yoabu, “Nimemwona Absalomu akininginia kwenye mwaloni.”

11. Yoabu akamwambia mtu huyo, “Nini? Ulimwona Absalomu? Kwa nini, basi, hukumpiga papo hapo hadi ardhini? Ningefurahi kukulipa vipande kumi vya fedha na mkanda.”

12. Lakini yule mtu akamwambia Yoabu, “Hata kama ningeuona uzito wa vipande 1,000 vya fedha mkononi mwangu, nisingeunyosha mkono wangu dhidi ya mwana wa mfalme. Maana, tulimsikia mfalme alipokuamuru wewe Abishai na Itai kwamba, kwa ajili yake, mumlinde kijana Absalomu.

13. Kwa upande mwingine, kama ningemtendea kwa hila (na hakuna lolote linalofichika kwa mfalme) wewe mwenyewe ungeniruka.”

14. Yoabu akamwambia, “Mimi sina wakati wa kupoteza pamoja nawe.” Hapo Yoabu akachukua mikuki midogo mitatu mkononi mwake, akaenda na kumchoma Absalomu moyoni, Absalomu akiwa bado hai kwenye tawi la mwaloni.

Kusoma sura kamili 2 Samueli 18