Agano la Kale

Agano Jipya

2 Samueli 11:16-27 Biblia Habari Njema (BHN)

16. Basi, Yoabu alipokuwa anauzingira mji alimweka Uria mahali ambapo alijua wazi wanajeshi wa adui walikuwa hodari sana.

17. Wakazi wa mji huo walitoka katika mji wao na kupigana na Yoabu. Baadhi ya watumishi wa Daudi, waliuawa. Uria Mhiti naye aliuawa pia.

18. Kisha, Yoabu alipeleka habari zote kwa Daudi akimweleza juu ya vita.

19. Yoabu akamwamuru huyo mtumishi aliyemtuma hivi, “Baada ya kumweleza mfalme mambo yote kuhusu vita,

20. akikasirika na kukuuliza, ‘Kwa nini mlikwenda karibu na mji mlipokuwa mnapigana? Hamkujua kwamba wangewapiga mishale kutoka kwenye kuta za mji wao?

21. Nani alimuua Abimeleki mwana wa Yerubeshethi? Si alikuwa mwanamke mmoja mjini Thebesi ambaye alitupa jiwe la kusagia kutoka kwenye ukuta nalo likamuua Abimeleki? Kwa nini basi, mlikwenda karibu na ukuta?’ Basi, wewe utamwambia hivi, ‘Hata mtumishi wako Uria Mhiti, naye amekufa.’”

22. Yule mjumbe alikwenda kwa Daudi na kumwambia yote aliyotumwa na Yoabu ayaseme.

23. Yule mjumbe akamwambia Daudi, “Adui zetu walituzidi nguvu, wakatoka nje ya miji na kutushambulia nyikani. Hata hivyo sisi tuliwarudisha mpaka kwenye lango la mji.

24. Halafu wakatupiga mishale sisi watumishi wako kutoka ukutani. Baadhi ya watumishi wako waliuawa. Hata mtumishi wako Uria, Mhiti, naye amekufa.”

25. Daudi akamwambia yule mjumbe, “Utamwambia hivi Yoabu, ‘Jambo hili lisikusumbue kwani upanga hauna macho, vita huua yeyote yule. Bali, imarisha mashambulizi dhidi ya mji, hadi umeuangamiza mji huo’. Ndivyo utakavyomtia moyo Yoabu.”

26. Bathsheba mke wa Uria aliposikia kwamba mumewe Uria amekufa, alimwombolezea mumewe.

27. Muda wa matanga ulipokwisha, Daudi aliagiza Bathsheba achukuliwe na kupelekwa nyumbani kwake. Bathsheba akawa mke wa Daudi, naye akamzalia Daudi mtoto wa kiume. Lakini jambo hilo alilofanya Daudi lilimchukiza Mwenyezi-Mungu.

Kusoma sura kamili 2 Samueli 11