Agano la Kale

Agano Jipya

2 Samueli 10:8-17 Biblia Habari Njema (BHN)

8. Waamoni walitoka na kujipanga tayari kwa vita kwenye lango la mji wa Raba, mji wao mkuu; nao Waaramu kutoka Soba na Rehobu na watu kutoka Tobu na Maaka walijipanga nyikani.

9. Yoabu alipoona kuwa vita ni vikali dhidi yake, mbele na nyuma, aliwateua baadhi ya wanajeshi Waisraeli hodari zaidi akawapanga kukabiliana na Waaramu.

10. Wale wanajeshi wengine waliobaki aliwaweka chini ya uongozi wa ndugu yake Abishai, naye akawapanga ili wakabiliane na Waamoni.

11. Yoabu akamwambia Abishai, “Ikiwa Waaramu wananizidi nguvu, utanisaidia lakini kama Waamoni wanakuzidi nguvu, nitakuja kukusaidia.

12. Lakini jipe moyo! Tupigane kiume kwa ajili ya watu wetu na kwa ajili ya miji ya Mungu wetu; naye Mwenyezi-Mungu atutendee lile analoona ni jema kwake.”

13. Basi, Yoabu na watu wake walisonga mbele kwenda kupigana na Waaramu, nao Waaramu walikimbia.

14. Waamoni walipoona kuwa Waaramu wamekimbia, nao pia walimkimbia Abishai na kuingia mjini. Yoabu akaacha kupigana na Waamoni, akarudi Yerusalemu.

15. Lakini Waaramu walipoona kwamba wameshindwa na Waisraeli, walijikusanya pamoja.

16. Hadadezeri aliagiza Waaramu waliokuwa ngambo ya mto Eufrate waletwe, wapelekwe huko Helamu wakiongozwa na Shobaki kamanda wa jeshi la Hadadezeri.

17. Daudi alipopata habari, aliwakusanya pamoja Waisraeli wote, akavuka mto Yordani na kwenda mpaka Helamu. Nao Waaramu walijipanga tayari kwa vita dhidi ya Daudi, wakaanza kupigana naye.

Kusoma sura kamili 2 Samueli 10