Agano la Kale

Agano Jipya

2 Mambo Ya Nyakati 34:4-17 Biblia Habari Njema (BHN)

4. Watu wake walizibomoa madhabahu za ibada za Mabaali mbele yake na alizikatakata madhabahu za kufukizia ubani zilizoinuliwa juu ya madhabahu hizo; pia alizipondaponda sanamu za Ashera na nyinginezo za kuchonga na za kusubu; alizifanya kuwa mavumbi, nayo mavumbi akayamwaga juu ya makaburi ya wale ambao hapo awali walizitolea sadaka.

5. Aidha, aliiteketeza mifupa ya makuhani wa miungu hiyo kwenye madhabahu zao, hivyo akatakasa Yuda na Yerusalemu.

6. Alifanya vivyo hivyo katika miji ya Manase, Efraimu, Simeoni mpaka Naftali na kwenye magofu yaliyokuwa kandokando ya miji hiyo.

7. Alizibomoa madhabahu na kupondaponda Maashera na sanamu za kuchongwa zikawa mavumbi. Kadhalika alizikatakata madhabahu za kufukizia ubani katika nchi yote ya Israeli. Hatimaye alirudi Yerusalemu.

8. Katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wake, wakati ambapo alikuwa amekwisha takasa nchi na nyumba, alituma watu watatu: Shafani mwana wa Azalia, Maaseya gavana wa mji na Yoa mwana wa Yoahazi, Katibu, ili waende kuirekebisha nyumba ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wake.

9. Walimwendea Hilkia, kuhani mkuu, wakamkabidhi fedha zilizokuwa zimeletwa katika nyumba ya Mungu ambazo zilikusanywa na Walawi wangojamlango, kutoka Manase, Efraimu na kutoka pande nyingine zote za Israeli, nchi yote ya Yuda na Benyamini, na pia kutoka kwa wenyeji wa Yerusalemu.

10. Zilikabidhiwa wale mafundi waliosimamia marekebisho ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu; na mafundi waliofanya kazi katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu walizitoa ili kutengeneza na kurekebisha nyumba.

11. Waliwapatia maseremala na wajenzi kwa ajili ya kununulia mawe yaliyochongwa, mbao za kuunganishia na mihimili ya kutumia katika kurekebisha yale majengo ambayo wafalme wa Yuda waliyaacha yakabomokabomoka.

12. Watu hao waliifanya kazi hiyo kwa uaminifu, wakiwa chini ya uongozi wa Walawi Yahathi na Obadia, chini ya wana wa Merari na Zekaria na Meshulamu na chini ya wazawa wa Kohathi. Walawi wote waliokuwa na ujuzi sana katika upigaji wa vyombo vya muziki,

13. waliwasimamia wachukuzi wa mizigo na kuwaongoza wote waliofanya kazi mbalimbali; baadhi ya Walawi walikuwa waandishi, maofisa na hata walinda mlango.

14. Wakati walipokuwa wanashughulika na utoaji wa fedha zilizokuwa zimeletwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, kuhani Hilkia alipata Kitabu cha Sheria ya Mwenyezi-Mungu iliyotolewa kwa mkono wa Mose.

15. Kisha Hilkia alimwambia Shafani mwandishi, “Nimekipata Kitabu cha Sheria katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu.” Halafu Hilkia akampatia Shafani kitabu.

16. Naye Shafani akampelekea mfalme na kumpasha habari, akisema, “Yote watumishi wako waliyokabidhiwa wanayafanya.

17. Wametoa fedha zilizopatikana katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, halafu wamezikabidhi kwa wasimamizi na mafundi.”

Kusoma sura kamili 2 Mambo Ya Nyakati 34