Agano la Kale

Agano Jipya

2 Mambo Ya Nyakati 34:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Yosia alikuwa na umri wa miaka minane alipoanza kutawala; alitawala miaka thelathini na mmoja huko Yerusalemu.

2. Alitenda mema mbele ya Mwenyezi-Mungu. Alifuata njia zake Daudi babu yake, na kushika amri za Mwenyezi-Mungu kwa dhati.

3. Katika mwaka wa nne wa utawala wake, mfalme Yosia, akiwa bado kijana, alianza kumwabudu Mungu wa Daudi, baba yake. Baadaye alipokuwa na umri wa miaka kumi na miwili alianza kuisafisha Yuda na Yerusalemu kwa kuharibu mahali pa kuabudia miungu mingine, sanamu za Ashera, na sanamu nyinginezo za kuchonga na za kusubu.

4. Watu wake walizibomoa madhabahu za ibada za Mabaali mbele yake na alizikatakata madhabahu za kufukizia ubani zilizoinuliwa juu ya madhabahu hizo; pia alizipondaponda sanamu za Ashera na nyinginezo za kuchonga na za kusubu; alizifanya kuwa mavumbi, nayo mavumbi akayamwaga juu ya makaburi ya wale ambao hapo awali walizitolea sadaka.

5. Aidha, aliiteketeza mifupa ya makuhani wa miungu hiyo kwenye madhabahu zao, hivyo akatakasa Yuda na Yerusalemu.

6. Alifanya vivyo hivyo katika miji ya Manase, Efraimu, Simeoni mpaka Naftali na kwenye magofu yaliyokuwa kandokando ya miji hiyo.

7. Alizibomoa madhabahu na kupondaponda Maashera na sanamu za kuchongwa zikawa mavumbi. Kadhalika alizikatakata madhabahu za kufukizia ubani katika nchi yote ya Israeli. Hatimaye alirudi Yerusalemu.

8. Katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wake, wakati ambapo alikuwa amekwisha takasa nchi na nyumba, alituma watu watatu: Shafani mwana wa Azalia, Maaseya gavana wa mji na Yoa mwana wa Yoahazi, Katibu, ili waende kuirekebisha nyumba ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wake.

9. Walimwendea Hilkia, kuhani mkuu, wakamkabidhi fedha zilizokuwa zimeletwa katika nyumba ya Mungu ambazo zilikusanywa na Walawi wangojamlango, kutoka Manase, Efraimu na kutoka pande nyingine zote za Israeli, nchi yote ya Yuda na Benyamini, na pia kutoka kwa wenyeji wa Yerusalemu.

10. Zilikabidhiwa wale mafundi waliosimamia marekebisho ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu; na mafundi waliofanya kazi katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu walizitoa ili kutengeneza na kurekebisha nyumba.

Kusoma sura kamili 2 Mambo Ya Nyakati 34