Agano la Kale

Agano Jipya

2 Mambo Ya Nyakati 32:8-21 Biblia Habari Njema (BHN)

8. Yeye anazo nguvu za kibinadamu tu, hali sisi tunaye Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, kutusaidia na kutupigania vita vyetu.” Maneno haya ya mfalme Hezekia yaliwatia moyo sana watu hao.

9. Baada ya hayo, Senakeribu mfalme wa Ashuru, ambaye bado alikuwa ameuzingira mji wa Lakishi akiwa na majeshi yake yote, aliwatuma watumishi wake Yerusalemu kwa Hezekia mfalme wa Yuda na kwa watu wote wa Yuda waliokuwa Yerusalemu, akisema

10. “Hivi ndivyo anavyosema Senakeribu mfalme wa Ashuru: Je, mnategemea nini hata mnakaa Yerusalemu, mji ambao umezingirwa?

11. Je, si kana kwamba Hezekia anawadanganya ili awafanye mfe kwa njaa au kiu anapowaambia, ‘Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu atawaokoa mikononi mwa mfalme wa Ashuru?’

12. Je, siye huyu Hezekia aliyepaharibu mahali pake pa kuabudia na madhabahu zake na kuwaamuru watu wote wa Yuda na Yerusalemu akisema: ‘Mtaabudu mbele ya madhabahu moja, na juu yake mtateketeza sadaka zenu?’

13. Je, kwani hamjui yale yote ambayo mimi na babu zangu tumewatenda watu wote wa mataifa mengine? Je, miungu ya mataifa ya nchi hizo iliweza kuzikomboa nchi zao mkononi mwangu?

14. Ni mungu gani kati ya miungu ya mataifa hayo iliyoharibiwa kabisa na babu zangu aliyeweza kuwakomboa watu wake kutoka mikononi mwangu ndio nanyi muwe na tumaini ya kwamba Mungu wenu atawaokoeni mikononi mwangu?

15. Msidanganywe na Hezekia wala msishawishike kwa hayo. Msimwamini mtu huyu, kwa maana hapajatokea mungu wa taifa au mfalme yeyote aliyefaulu kuwakomboa watu wake kutoka mikononi mwa mfalme wa Ashuru, sembuse huyu Mungu wenu!”

16. Watumishi wa mfalme wa Ashuru walisema maneno mengine mengi mabaya dhidi ya Mwenyezi-Mungu, na dhidi ya Hezekia mtumishi wake.

17. Mfalme mwenyewe aliandika barua akamtukana na kumdharau Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, akisema, “Kama vile ambavyo miungu ya mataifa mengine haikuweza kuwaokoa watu wao kutoka mikononi mwangu, vivyo hivyo Mungu wa Hezekia hataweza kuwaokoa watu wake.”

18. Maofisa hao waliwaambia kwa sauti kubwa kwa lugha ya Kiebrania watu wa Yerusalemu waliokuwa ukutani, wakikusudia kuwatia hofu na woga ili wauteke mji kwa urahisi.

19. Wakazungumza juu ya Mungu wa Yerusalemu kana kwamba ni miungu ya mataifa mengine; sanamu tu zilizotengenezwa kwa mikono ya wanadamu!

20. Hapo mfalme Hezekia na nabii Isaya, mwana wa Amozi, wakamwomba Mungu na kumlilia awasaidie kwa ajili ya mambo haya.

21. Naye Mwenyezi-Mungu akatuma malaika, akaenda na kuwakatilia mbali mashujaa, wanajeshi, makamanda na maofisa katika kambi ya mfalme wa Ashuru. Basi, mfalme wa Ashuru akarejea nchini mwake amejawa aibu. Mara alipoingia ndani ya nyumba ya mungu wake, baadhi ya wanawe mwenyewe wakamuua papo hapo kwa upanga.

Kusoma sura kamili 2 Mambo Ya Nyakati 32