Agano la Kale

Agano Jipya

2 Mambo Ya Nyakati 29:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Hezekia alianza kutawala Yuda akiwa na umri wa miaka ishirini na mitano, akatawala huko Yerusalemu kwa muda wa miaka ishirini na tisa. Mama yake alikuwa Abiya binti Zekaria.

2. Alitenda mema mbele ya Mwenyezi-Mungu, kama vile alivyofanya Daudi, babu yake.

3. Mnamo mwezi wa kwanza wa mwaka wa kwanza wa utawala wake, mfalme Hezekia aliifungua tena milango ya hekalu, akaitengeneza.

4. Aliwaingiza makuhani na Walawi, kisha akawakusanya uani upande wa mashariki,

5. akawaambia, “Nisikieni enyi Walawi! Jitakaseni na itakaseni nyumba ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zenu. Toeni uchafu wote uliomo patakatifu.

6. Kwa maana babu zetu waliasi na kutenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu. Wamemwacha, wakageuzia mbali nyuso zao na kupawekea kisogo mahali aishipo Mwenyezi-Mungu.

7. Tena, waliifunga milango ya ukumbi, wakazizima taa, na hawajafukiza ubani wala kutoa tambiko za kuteketeza katika mahali patakatifu pa Mungu wa Israeli.

8. Kwa sababu hii, Mwenyezi-Mungu aliikasirikia sana Yuda na Yerusalemu, na yale aliyowatenda yamewashangaza na kuwaogofya watu wote, wakawazomea. Haya yote mmeyaona wenyewe kwa macho yenu.

9. Baba zetu waliuawa vitani, na wana wetu na binti zetu na wake zetu ni mateka kwa sababu hiihii.

10. Sasa, nimeamua kwa dhati kufanya agano na Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, ili asitukasirikie zaidi.

11. Basi wanangu, muwe na nidhamu. Mwenyezi-Mungu amewachagua nyinyi ili mumtumikie, muwaongoze watu wake katika ibada, na kumfukizia ubani.”

Kusoma sura kamili 2 Mambo Ya Nyakati 29