Agano la Kale

Agano Jipya

2 Mambo Ya Nyakati 28:5-21 Biblia Habari Njema (BHN)

5. Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, alimwacha mfalme Ahazi ashindwe na mfalme wa Aramu ambaye pia alichukua mateka watu wake wengi, akarudi nao Damasko. Kadhalika, alimfanya ashindwe na Peka, mwana wa Remalia, mfalme wa Israeli, ambaye alimshinda na kuua watu wengi sana.

6. Aliua askari mashujaa wa Yuda 120,000 katika siku moja. Ilitokea hivyo kwa sababu walimwacha Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zao.

7. Zikri, askari mmoja shujaa wa Israeli, alimuua Maaseya, mwana wa mfalme, Azrikamu, kamanda wa Ikulu, na Elkana aliyekuwa mtu wa pili chini ya mfalme.

8. Jeshi la Israeli lilichukua mateka ndugu zao watu laki mbili wakiwemo wanawake na watoto. Waliwachukua hadi Samaria pamoja na mali nyingi waliyoteka nyara.

9. Baadaye kidogo mtu mmoja, jina lake Odedi, nabii wa Mwenyezi-Mungu, alikuwa anakaa Samaria. Yeye alitoka kuwalaki wanajeshi wa Israeli pamoja na mateka wao wa Yuda walipokuwa karibu kuingia Samaria, akawaambia, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zenu, alikuwa amewakasirikia watu wa Yuda, ndiyo maana akawatia mikononi mwenu lakini mmewaua kwa hasira. Tendo hilo limefika mbinguni.

10. Sasa mnanuia kuwafanya wanaume na wanawake wa Yuda na Yerusalemu watumwa wenu. Je, hamtambui ya kuwa nyinyi pia mmetenda dhambi dhidi ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu?

11. Sasa sikieni yale nisemayo: Warudisheni ndugu zenu na dada zenu mliowateka, maana ghadhabu kali ya Mwenyezi-Mungu iko juu yenu.”

12. Nao wakuu fulani wa Efraimu, Azaria mwana wa Yohanani, Berekia mwana wa Meshilemothi, Yehizkia mwana wa Shalumu na Amasa mwana wa Hadlai, pia waliwashutumu hao waliotoka vitani.

13. Wakawaambia, “Msiwalete humu mateka hao, kwa sababu mnanuia kutuletea hatia mbele ya Mwenyezi-Mungu; tendo hili huku litakuwa nyongeza ya dhambi yetu na hatia yetu; kwa sababu hatia yetu tayari ni kubwa na kuna ghadhabu kali juu ya Israeli.”

14. Hivyo, wanajeshi waliwaacha mateka wao na nyara zote mbele ya wakuu na mkutano wote.

15. Wale wakuu waliotajwa majina yao waliwachukua mateka na kwa kutumia nyara wakawavika mateka ambao hawakuwa na nguo; waliwapatia ndara, chakula na vinywaji, na kuwapaka mafuta. Wale ambao walikuwa hawajiwezi, wakawabeba kwa punda, wakawachukua mateka wote hadi Yeriko, mji wa mitende, kwa ndugu zao; kisha wao wakarudi Samaria.

16. Wakati huo, mfalme Ahazi alituma wajumbe kwa mfalme wa Ashuru kuomba msaada,

17. kwa sababu Waedomu walikuwa wamekuja tena, wakaivamia nchi ya Yuda, wakawashinda na kuchukua mateka wengi.

18. Wakati huohuo pia, Wafilisti walikuwa wakiishambulia miji ya Shefela na Negebu ya Yuda. Waliiteka miji ya Beth-shemeshi, Ayaloni, Gederothi, Soko na vijiji vyake, Timna na vijiji vyake, Gimzo na vijiji vyake, wakafanya makao yao huko.

19. Kwa sababu mfalme Ahazi wa Israeli alikuwa na ukatili kwa watu wake, na alikosa uaminifu kwa Mwenyezi-Mungu, Mwenyezi-Mungu aliwafanya watu wa Yuda wakose nguvu.

20. Tiglath-pileseri, mfalme wa Ashuru alimshambulia badala ya kumtia nguvu.

21. Ahazi alichukua dhahabu kutoka katika nyumba ya Mungu, kutoka ikulu na nyumba za wakuu, akampa mfalme wa Ashuru kama kodi; lakini hili pia halikumsaidia kitu.

Kusoma sura kamili 2 Mambo Ya Nyakati 28