Agano la Kale

Agano Jipya

2 Mambo Ya Nyakati 24:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Yoashi alikuwa na umri wa miaka saba alipoanza kutawala. Alitawala kwa muda wa miaka arubaini huko Yerusalemu. Mama yake alikuwa Sibia kutoka Beer-sheba.

2. Wakati wote kuhani Yehoyada alipokuwa hai Yoashi alitenda mema mbele ya Mwenyezi-Mungu.

3. Yehoyada akamwoza wake wawili, nao wakamzalia watoto wa kiume na wa kike.

4. Baadaye Yoashi aliamua kurekebisha nyumba ya Mwenyezi-Mungu.

5. Basi, akawaita makuhani na Walawi na kuwaamuru, “Nendeni katika miji ya Yuda, mkusanye fedha kutoka kwa Waisraeli wote ili kurekebisha nyumba ya Mungu wenu kila mwaka; harakisheni.” Lakini Walawi hawakuharakisha.

6. Basi, mfalme akamwita kiongozi Yehoyada, akamwuliza, “Mbona hujaamrisha Walawi kukusanya kutoka kwa watu wa Yuda na Yerusalemu, kodi ambayo Mose mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, aliagiza watu walipe kwa ajili ya Hema Takatifu la Mwenyezi-Mungu?”

7. (Athalia yule mwanamke mwovu na wafuasi wake walivunja nyumba ya Mungu na kuingia ndani; na vyombo vitakatifu vya nyumba ya Mwenyezi-Mungu walivitumia katika ibada za Mabaali.)

8. Basi, mfalme aliwaamuru Walawi, wakatengeneza sanduku la matoleo na kuliweka nje ya lango la nyumba ya Mwenyezi-Mungu.

9. Kisha tangazo likatolewa kote katika Yuda na Yerusalemu, kwamba watu wote wamletee Mwenyezi-Mungu kodi ambayo Mose mtumishi wa Mungu, aliwaamuru Waisraeli walipokuwa jangwani.

10. Wakuu wote na watu wote walifurahi wakaleta kodi yao wakaitumbukiza kwenye sanduku mpaka walipomaliza kufanya hivyo.

Kusoma sura kamili 2 Mambo Ya Nyakati 24