Agano la Kale

Agano Jipya

2 Mambo Ya Nyakati 21:12-20 Biblia Habari Njema (BHN)

12. Nabii Elia alimpelekea mfalme Yehoramu barua ifuatayo:“Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Daudi babu yako, anakulaani kwa sababu hukufuata mwenendo wa Yehoshafati baba yako, au wa Asa mfalme wa Yuda.

13. Badala yake umeifuata mienendo ya wafalme wa Israeli na kuwaongoza watu wa Yuda na Yerusalemu katika kukosa uaminifu kama vile Ahabu, na wafalme wa jamaa yake waliomfuata walivyowaongoza watu wa Israeli kukosa uaminifu. Pia umewaua ndugu zako, ndugu za baba mmoja waliokuwa watu wema zaidi kuliko wewe.

14. Kwa sababu hiyo, Mwenyezi-Mungu atawaadhibu vikali watu wako, wanao, wake zako na kuiharibu mali yako yote.

15. Wewe mwenyewe utaugua maradhi mabaya ya tumbo, ambayo yataongezeka siku hata siku, mpaka matumbo yako yatoke nje.”

16. Kulikuwa na Wafilisti na Waarabu wengine waliokuwa wakikaa karibu na Waethiopia. Hawa, Mwenyezi-Mungu aliwapandisha hasira ili wapigane na Yehoramu.

17. Basi, wakaishambulia nchi ya Yuda, wakaiteka mali yote iliyokuwamo katika jumba la mfalme na kuwachukua mateka wanawe wote na wake zake, isipokuwa Ahazia, mwanawe mdogo.

18. Baada ya haya yote, Mwenyezi-Mungu akamletea mfalme ugonjwa wa tumbo usioponyeka.

19. Aliendelea kuugua, na ugonjwa wake ukawa unaongezeka siku hata siku, hata kufikia mwisho wa mwaka wa pili, akafariki dunia katika maumivu makali. Watu hawakuwasha moto kuomboleza kifo chake kama walivyowafanyia babu zake.

20. Yehoramu alianza kutawala akiwa na umri wa miaka thelathini na miwili; akatawala huko Yerusalemu kwa muda wa miaka minane. Wakati alipofariki, hakuna mtu yeyote aliyemsikitikia. Alizikwa katika mji wa Daudi, ila si katika makaburi ya wafalme.

Kusoma sura kamili 2 Mambo Ya Nyakati 21