Agano la Kale

Agano Jipya

2 Mambo Ya Nyakati 18:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Wakati mfalme Yehoshafati wa Yuda alipokuwa amekwisha kuwa mtu tajiri na mwenye heshima, alifanya mpango wa ndoa baina ya jamaa yake, na jamaa ya mfalme Ahabu wa Israeli.

2. Baada ya miaka kadhaa Yehoshafati alikwenda Samaria kumtembelea mfalme Ahabu. Ahabu akamchinjia Yehoshafati kondoo na ng'ombe wengi, kwa heshima yake pamoja na watu waliokuwa pamoja naye, kisha akamshawishi aandamane naye kuushambulia mji wa Ramoth-gileadi.

3. Ahabu mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati mfalme wa Yuda, “Je, utaandamana nami kwenda kuushambulia mji wa Ramoth-gileadi?” Naye akajibu, “Naam, mimi niko nawe, pia watu wangu ni watu wako. Tutakuwa pamoja nawe vitani.”

4. Kisha Yehoshafati akaendelea kumwambia mfalme wa Israeli, “Lakini kwanza mwulize Mwenyezi-Mungu shauri.”

5. Basi, Ahabu akaitisha kikao cha manabii wapatao 400, akawauliza, “Je, twende tukaushambulie mji wa Ramoth-gileadi, au nisiende?” Wao wakamjibu, “Nenda! Mungu atakupatia ushindi!”

6. Lakini, Yehoshafati akauliza, “Je, hapa hakuna nabii mwingine wa Mwenyezi-Mungu ambaye twaweza kumwuliza shauri?”

7. Naye mfalme wa Israeli akamjibu Yehoshafati, “Yupo bado mmoja, Mikaya mwana wa Imla. Yeye twaweza kumwuliza shauri la Mwenyezi-Mungu. Lakini namchukia kwa sababu yeye kamwe hatabiri jambo jema juu yangu, ila mabaya tu.” Yehoshafati akamwambia, “Si vizuri mfalme kusema hivyo.”

8. Basi, Ahabu, mfalme wa Israeli akamwita ofisa mmoja na kumwamuru, “Haraka, nenda ukamlete Mikaya mwana wa Imla.”

9. Wakati huo, mfalme wa Israeli pamoja na Yehoshafati, mfalme wa Yuda, walikuwa wameketi katika viti vyao vya enzi wakikaa kwenye kiwanja cha kupuria nafaka kwenye lango la kuingilia mjini Samaria nao walikuwa wamevalia mavazi yao ya kifalme. Wakati huo manabii wote walikuwa wakitoa unabii wao mbele yao.

10. Kisha mmoja wa manabii hao, Sedekia mwana wa Kenaana, akajitengenezea pembe za chuma, akasema, “Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Kwa pembe hizi, utawarudisha nyuma Washamu hata kuwaangamiza.’”

11. Hata wale manabii wengine wakatabiri vivyo hivyo wakasema, “Nenda ukaushambulie Ramoth-gileadi, Mwenyezi-Mungu atautia mikononi mwako.”

12. Wakati huo, yule mjumbe aliyetumwa kwa Mikaya alimwambia, “Manabii wengine wote kwa pamoja wamemtabiria mfalme ushindi; tafadhali nawe pia ufanye kama wao, umtabirie mema.”

Kusoma sura kamili 2 Mambo Ya Nyakati 18