Agano la Kale

Agano Jipya

2 Mambo Ya Nyakati 14:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Mwishowe, Abiya alifariki na kuzikwa katika mji wa Daudi na Asa mwanawe akatawala mahali pake. Wakati wa Asa, kulikuwa na amani nchini kwa muda wa miaka kumi.

2. Asa alitenda yaliyokuwa mazuri na mema mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wake.

3. Aliondoa nchini madhabahu za kigeni na mahali pa kuabudia miungu mingine, akabomoa minara na kuzikatakata sanamu za Ashera.

4. Aliwaamuru watu wa Yuda wamtafute Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zao, na kuzitii sheria na amri.

5. Pia aliondoa mahali pote pa kuabudia miungu mingine na meza za kufukizia ubani kutoka katika miji yote ya Yuda; halafu ufalme wake ulikuwa na amani chini ya utawala wake.

6. Alijenga miji yenye ngome katika Yuda wakati huo wa amani, na kwa muda wa miaka kadhaa, hapakutokea vita kwa maana Mwenyezi-Mungu alimpa amani.

7. Naye akawaambia watu wa Yuda, “Na tuiimarishe miji kwa kuizungushia kuta na minara na malango yenye makomeo. Nchi bado imo mikononi mwetu kwa maana tumeyatenda mapenzi yake Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, naye ametupa amani pande zote.” Basi wakajenga, wakafanikiwa.

8. Mfalme Asa alikuwa na jeshi la askari 300,000 kutoka Yuda, wenye ngao na mikuki, na wengine 280,000 kutoka Benyamini, wenye ngao na pinde. Wote walikuwa watu mashujaa sana.

9. Zera, Mwethiopia aliishambulia nchi ya Yuda akiwa na jeshi la askari 1,000,000 na magari 300, akasonga mbele hadi Maresha.

Kusoma sura kamili 2 Mambo Ya Nyakati 14