Agano la Kale

Agano Jipya

2 Mambo Ya Nyakati 12:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Ikawa utawala wa Rehoboamu ulipokwisha imarika na kuwa na nguvu, yeye pamoja na watu wake wote waliacha kutii sheria ya Mwenyezi-Mungu.

2. Katika mwaka wa tano wa utawala wake, kwa sababu hawakumtii Mwenyezi-Mungu, Shishaki, mfalme wa Misri aliushambulia Yerusalemu,

3. akiwa na magari 1,200, wapandafarasi 60,000, na askari wengi mno wasiohesabika, waliotoka Misri pamoja naye: Walibia, Wasukii na Waethiopia.

4. Aliiteka miji yenye ngome katika Yuda, akafika hadi Yerusalemu.

5. Kisha Nabii Shemaya alimwendea mfalme Rehoboamu na wakuu wa Yuda, waliokusanyika Yerusalemu ambapo walikimbilia ili kumwepuka Shishaki, akamwambia, “Mwenyezi-Mungu asema hivi, ‘Nyinyi mmeniacha mimi, kwa hiyo basi, nami nimewaacha nyinyi na kuwatia mikononi mwa Shishaki.’”

6. Ndipo wakuu wa Israeli na mfalme wakajinyenyekesha, wakasema, “Mwenyezi-Mungu ametenda sawa.”

7. Mwenyezi-Mungu alipoona ya kuwa wamejinyenyekesha, alizungumza tena na nabii Shemaya, akamwambia, “Wamejinyenyekesha, sitawaangamiza, bali nitawaokoa baada ya muda mfupi. Sitaushushia mji wa Yerusalemu ghadhabu yangu kuuharibu kwa mkono wa Shishaki,

8. lakini watamtumikia ili wapate kujua tofauti iliyopo kati ya kunitumikia mimi na kuwatumikia wafalme wa duniani.”

Kusoma sura kamili 2 Mambo Ya Nyakati 12