Sura

  1. 1
  2. 2
  3. 3
  4. 4
  5. 5
  6. 6
  7. 7
  8. 8
  9. 9
  10. 10
  11. 11
  12. 12
  13. 13
  14. 14
  15. 15
  16. 16
  17. 17
  18. 18
  19. 19
  20. 20
  21. 21
  22. 22
  23. 23
  24. 24
  25. 25
  26. 26
  27. 27
  28. 28
  29. 29
  30. 30
  31. 31
  32. 32
  33. 33
  34. 34
  35. 35
  36. 36

Agano la Kale

Agano Jipya

2 Mambo Ya Nyakati 12 Biblia Habari Njema (BHN)

Wamisri waivamia Yuda

1. Ikawa utawala wa Rehoboamu ulipokwisha imarika na kuwa na nguvu, yeye pamoja na watu wake wote waliacha kutii sheria ya Mwenyezi-Mungu.

2. Katika mwaka wa tano wa utawala wake, kwa sababu hawakumtii Mwenyezi-Mungu, Shishaki, mfalme wa Misri aliushambulia Yerusalemu,

3. akiwa na magari 1,200, wapandafarasi 60,000, na askari wengi mno wasiohesabika, waliotoka Misri pamoja naye: Walibia, Wasukii na Waethiopia.

4. Aliiteka miji yenye ngome katika Yuda, akafika hadi Yerusalemu.

5. Kisha Nabii Shemaya alimwendea mfalme Rehoboamu na wakuu wa Yuda, waliokusanyika Yerusalemu ambapo walikimbilia ili kumwepuka Shishaki, akamwambia, “Mwenyezi-Mungu asema hivi, ‘Nyinyi mmeniacha mimi, kwa hiyo basi, nami nimewaacha nyinyi na kuwatia mikononi mwa Shishaki.’”

6. Ndipo wakuu wa Israeli na mfalme wakajinyenyekesha, wakasema, “Mwenyezi-Mungu ametenda sawa.”

7. Mwenyezi-Mungu alipoona ya kuwa wamejinyenyekesha, alizungumza tena na nabii Shemaya, akamwambia, “Wamejinyenyekesha, sitawaangamiza, bali nitawaokoa baada ya muda mfupi. Sitaushushia mji wa Yerusalemu ghadhabu yangu kuuharibu kwa mkono wa Shishaki,

8. lakini watamtumikia ili wapate kujua tofauti iliyopo kati ya kunitumikia mimi na kuwatumikia wafalme wa duniani.”

9. Basi, mfalme Shishaki wa Misri aliushambulia Yerusalemu, akaichukua hazina yote ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu na ya ikulu, pamoja na ngao za dhahabu alizozitengeneza mfalme Solomoni.

10. Badala ya ngao hizo, mfalme Rehoboamu alitengeneza ngao za shaba na kuziweka chini ya ulinzi wa wangojamlango wa ikulu.

11. Kila wakati mfalme alipokwenda katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, walinzi waliiingia wakazibeba ngao hizo na baadaye wakazirudisha katika chumba cha ulinzi.

12. Alipojinyenyekesha, Mwenyezi-Mungu aliacha kumghadhibikia na hakumwangamiza kabisa. Zaidi ya hayo, hali ya nchi ya Yuda ilikuwa nzuri.

Muhtasari wa utawala wa Rehoboamu

13. Hivyo mfalme Rehoboamu alijiimarisha zaidi katika Yerusalemu, akaitawala Yuda. Alikuwa na umri wa miaka arubaini na mmoja alipoanza kutawala Yuda. Naye alitawala kwa muda wa miaka kumi na saba katika Yerusalemu, mji ambao Mwenyezi-Mungu aliuchagua miongoni mwa makabila yote ya Israeli aabudiwe humo. Mama yake Rehoboamu aliitwa Naama, kutoka Amoni.

14. Rehoboamu alitenda maovu, kwa maana hakunuia kumtafuta Mwenyezi-Mungu kwa moyo.

15. Matendo yote ya mfalme Rehoboamu ya mwanzo mpaka ya mwisho na rekodi ya ukoo yameandikwa katika kitabu cha Kumbukumbu za nabii Shemaya, na Kumbukumbu za Ido Mwonaji. Wakati huu wote, kulikuwa na vita vya mfululizo kati ya Rehoboamu na Yeroboamu.

16. Hatimaye Rehoboamu alifariki na kuzikwa katika mji wa Daudi, na Abiya mwanawe, akatawala mahali pake.