Agano la Kale

Agano Jipya

1 Wafalme 7:27-42 Biblia Habari Njema (BHN)

27. Hiramu pia alitengeneza magari kumi ya shaba, kila gari likiwa na urefu wa mita 1.75, upana wa mita 1.75, na kimo cha mita 1.25.

28. Magari hayo yalikuwa yameundwa hivi: Kulikuwa na mabamba ya chuma ambayo yalikuwa yameshikiliwa na mitalimbo. Juu ya mabamba hayo yaliyoshikiliwa na mitalimbo,

29. kulikuwa na sanamu za simba, mafahali na viumbe wenye mabawa. Sanamu hizo za simba na mafahali, zilikuwa zimefunikwa na kutandikwa mapambo yaliyosokotwa vizuri.

30. Isitoshe, kila gari lilikuwa na magurudumu manne ya shaba, na vyuma vya katikati vya kuyazungukia magurudumu hayo, vilikuwa vya shaba. Kwenye pembe nne za gari kulikuwa na vishikizo vya shaba kwa ajili ya birika kubwa. Karibu ya kila kishikio kuliwekwa mapambo ya maua ya kusokotwa.

31. Mlango wa gari ulikuwa katika sehemu iliyotokeza juu kwa kiasi cha nusu mita. Kwa nje, mlango ulikuwa umetiwa michoro; na mabamba yake yalikuwa ya mraba, si ya mviringo.

32. Na hayo magurudumu manne yalikuwa chini ya yale mabamba; vyuma vya katikati kuzunguka magurudumu hayo vilikuwa vimeunganishwa na mfumo wa gari lenyewe; na kimo cha magurudumu hayo kilikuwa sentimita 66.

33. Hayo magurudumu yalikuwa kama magurudumu ya magari ya kukokotwa; na vyuma vyake vya katikati, duara zake, mataruma yake na vikombe vyake: Hivyo vyote vilikuwa vya kusubu.

34. Chini ya kila gari kulikuwa na mihimili minne kwenye pembe zake, nayo ilishikamanishwa na gari.

35. Na juu ya kila gari palikuwa na utepe uliofanyiza duara ya kimo cha sentimita 22; na vishikio na mabamba yaliyokuwa upande wa juu yalishikamana na gari lenyewe.

36. Kwenye nafasi wazi iliyopatikana katika vishikio na mabamba ya kila gari, Hiramu alichonga michoro ya viumbe wenye mabawa, simba na miti ya mitende, akazungushia na mashada ya mapambo.

37. Mifano hiyo yote kumi ya magari ilifanana, ikiwa na kimo kimoja na muundo uleule.

38. Hiramu, pia alitengeneza mabirika kumi ya shaba, moja kwa kila gari. Kila birika ilikuwa na upana wa mita 1.75, na iliweza kuchukua maji kadiri ya lita 880.

39. Akaweka magari matano upande wa kusini wa nyumba, na matano upande wa kaskazini; na lile tangi akaliweka kwenye pembe ya kusini-mashariki ya nyumba.

40. Hiramu alitengeneza pia vyungu, sepetu na mabirika. Basi, Hiramu akamaliza kazi aliyoamriwa na mfalme Solomoni kuhusu nyumba ya Mwenyezi-Mungu:

41. Nguzo mbili, mabakuli mawili ya taji zilizowekwa juu ya nguzo, na nyavu mbili kwa ajili ya kufunika hizo taji mbili,

42. mifano ya makomamanga 400 kwa ajili ya nyavu hizo mbili, safu mbili za makomamanga kwa kila wavu ili kupamba zile taji mbili zilizokuwa juu ya nguzo.

Kusoma sura kamili 1 Wafalme 7