Agano la Kale

Agano Jipya

1 Wafalme 22:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Kwa muda wa miaka mitatu hivi, kulikuwa na amani kati ya Israeli na Aramu.

2. Lakini mnamo mwaka wa tatu, Yehoshafati, mfalme wa Yuda, alifika kumtembelea Ahabu, mfalme wa Israeli.

3. Ahabu akawaambia watumishi wake, “Je, hamjui kwamba Ramoth-gileadi ni mali yetu? Mbona basi tunajikalia tu bila kuunyakua kutoka kwa mfalme wa Aramu?”

4. Kisha akamwambia Yehoshafati, “Je, utaandamana nami kupigana huko Ramoth-gileadi?” Naye Yehoshafati akamjibu mfalme wa Israeli, “Naam; mimi na wewe ni kitu kimoja, na pia watu wangu ni watu wako, farasi wangu ni farasi wako.”

5. Kisha Yehoshafati aliendelea kumwambia mfalme wa Israeli: “Lakini, kwanza mwulize Mwenyezi-Mungu ushauri.”

6. Basi, Ahabu akaitisha kikao cha manabii wapatao 400, akawauliza, “Je, niende nikaushambulie mji wa Ramoth-gileadi au nisiende?” Wao wakamjibu: “Nenda! Mwenyezi-Mungu atakupatia ushindi.”

7. Lakini, Yehoshafati akasema, “Je, hapa hakuna nabii mwingine wa Mwenyezi-Mungu ambaye twaweza kumwuliza shauri?”

8. Naye mfalme wa Israeli akamjibu Yehoshafati, “Yupo, bado mmoja, Mikaya mwana wa Imla. Yeye twaweza kumwuliza shauri la Mwenyezi-Mungu. Lakini namchukia sana kwa sababu yeye, kamwe hatabiri jambo jema juu yangu, ila mabaya tu.” Yehoshafati akamwambia, “Si vizuri mfalme kusema hivyo.”

9. Basi, Ahabu, mfalme wa Israeli, akamwita mtumishi mmoja, akamwamuru, “Haraka! Nenda ukamlete Mikaya mwana wa Imla.”

10. Wakati huo, mfalme wa Israeli pamoja na Yehoshafati mfalme wa Yuda, walikuwa wameketi katika viti vyao vya enzi wakikaa kwenye kiwanja cha kupuria nafaka kwenye lango la kuingilia mjini Samaria nao walikuwa wamevalia mavazi yao ya kifalme; wakati huo manabii wote wakawa wanatabiri mbele yao.

11. Kisha mmoja wa manabii hao, Sedekia mwana wa Kenaana, akajitengenezea pembe za chuma akasema, “Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Kwa pembe hizi, utawarudisha nyuma Waaramu na kuwaangamiza.’”

Kusoma sura kamili 1 Wafalme 22