Agano la Kale

Agano Jipya

1 Wafalme 2:33-46 Biblia Habari Njema (BHN)

33. Adhabu ya mauaji hayo itakuwa juu ya Yoabu na wazawa wake milele. Bali Mwenyezi-Mungu atawapa ufanisi daima, Daudi na wazawa wake watakaokalia kiti chake cha enzi.”

34. Basi, Benaya mwana wa Yehoyada, akaenda hemani, akamuua Yoabu ambaye alizikwa shambani mwake, nyikani.

35. Mfalme akamweka Benaya mwana wa Yehoyada, kuwa jemadari wa jeshi mahali pa Yoabu, na Sadoki akawa kuhani mahali pa Abiathari.

36. Halafu mfalme akaagiza Shimei aitwe, akamwambia, “Jijengee nyumba humu Yerusalemu, ukae hapa bila kwenda mahali pengine popote pale.

37. Maana siku utakapotoka na kuvuka kijito Kidroni, nakuambia kweli utakufa, na kujilaumu wewe mwenyewe kwa kifo chako.”

38. Shimei akajibu, “Vema mfalme. Nitafanya kama ulivyosema.” Basi, akakaa Yerusalemu muda mrefu.

39. Lakini mwishoni mwa mwaka wa tatu, watumwa wawili wa Shimei walitoroka, wakaenda kwa Akishi mwana wa Maaka, mfalme wa Gathi. Habari zilipomfikia kwamba wako Gathi,

40. Shimei alipanda punda wake, akaenda huko kuwatafuta, kwa mfalme Akishi. Basi, akafika, akawapata, akawarudisha nyumbani.

41. Mfalme Solomoni alipopata habari kwamba Shimei alikuwa ametoka Yerusalemu, akaenda Gathi na kurudi,

42. alimwita Shimei na kumwambia, “Je, hukuniapia kwa jina la Mwenyezi-Mungu kwamba hutatoka Yerusalemu, nami sikukuonya kwa dhati kwamba, hakika utakufa kama utathubutu kwenda nje? Nawe ulikubali, ukaniambia, ‘Vema, nitatii.’

43. Mbona basi, umevunja kiapo chako kwa Mwenyezi-Mungu na kutojali amri niliyokupa?”

44. Mfalme aliendelea kumwambia Shimei, “Unayajua wazi maovu uliyomtendea baba yangu Daudi, na sasa, kwa sababu ya hayo, Mwenyezi-Mungu atakuadhibu.

45. Lakini mimi atanibariki, na kiti cha enzi cha Daudi kitaimarishwa mbele ya Mwenyezi-Mungu milele.”

46. Hapo, mfalme akamwamuru Benaya mwana wa Yehoyada, naye akatoka, akampiga na kumuua Shimei. Basi, ufalme ukaimarika chini ya Solomoni.

Kusoma sura kamili 1 Wafalme 2