Agano la Kale

Agano Jipya

1 Wafalme 19:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Mfalme Ahabu alimsimulia mkewe Yezebeli mambo yote aliyofanya Elia na jinsi alivyowaua manabii wa Baali kwa upanga.

2. Yezebeli akatuma mjumbe kwa Elia amwambie: “Miungu waniulie mbali, nakuapia, ikiwa saa hizi kesho sitakuwa nimekufanya kama mmoja wa hao manabii.”

3. Elia akakimbilia mjini Beer-sheba mkoani Yuda, alikomwacha mtumishi wake,

4. naye akatembea mwendo wa siku nzima kuingia jangwani. Basi, akafika, akaketi chini ya mti mmoja, mretemu. Hapo, akaomba afe, akisema, “Imetosha! Siwezi tena. Ee Mwenyezi-Mungu, sasa utoe uhai wangu. Mimi si bora kuliko wazee wangu.”

5. Basi, Elia akalala chini ya mti huo, akashikwa na usingizi. Punde, malaika akaja, akamgusa na kumwambia, “Amka ule.”

6. Elia alipotazama, akaona mkate uliookwa juu ya makaa, na chupa ya maji karibu na kichwa chake. Basi, akala, akanywa, akalala tena.

7. Malaika wa Mwenyezi-Mungu akamjia tena mara ya pili, akamgusa na kumwambia, “Amka ule, la sivyo safari itakuwa ngumu mno kwako.”

8. Elia akaamka, akala na kunywa. Kisha akatembea kwa nguvu ya chakula hicho mwendo wa siku arubaini, mchana na usiku, mpaka Horebu, mlima wa Mungu.

9. Huko, akafika penye pango, akakaa humo. Mara neno la Mwenyezi-Mungu likamjia: “Elia! Unafanya nini hapa?”

10. Naye akasema, “Naona uchungu na wivu, ewe Mwenyezi-Mungu, Mungu wa majeshi, kwa sababu watu wa Israeli wamevunja agano lako, wakazibomoa madhabahu zako na kuwaua manabii wako kwa upanga; ni mimi tu niliyebaki, nami pia wananiwinda, waniue!”

Kusoma sura kamili 1 Wafalme 19