Agano la Kale

Agano Jipya

1 Wafalme 18:3-15 Biblia Habari Njema (BHN)

3. Basi, Ahabu akamwita Obadia msimamizi wa ikulu. (Obadia alikuwa mtu amchaye Mwenyezi-Mungu sana,

4. na wakati Yezebeli alipowaua manabii wa Mwenyezi-Mungu, Obadia aliwachukua manabii 100, akawaficha hamsinihamsini pangoni, akawa anawapelekea chakula na maji).

5. Kisha, Ahabu akamwambia Obadia, “Labda tutapata majani na hapo tutawaokoa baadhi ya farasi na nyumbu wetu.”

6. Basi, wakagawana nchi ili wapate kuipitia yote; Ahabu akaenda upande mmoja na Obadia upande mwingine.

7. Obadia alipokuwa njiani, alikutana na Elia; naye Obadia alipomtambua Elia, aliinama chini na kusema, “Kumbe! Ni wewe bwana wangu Elia?”

8. Elia akamwambia, “Naam! Ni mimi Elia. Nenda ukamwambie bwana wako kwamba niko hapa.”

9. Obadia akasema, “Nimekosa nini hata utake kunitia hatarini ili niuawe na mfalme Ahabu?

10. Nakuapia kwa jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wako aliye hai, kwamba mfalme amekuwa akikutafuta duniani kote. Na mfalme yeyote akisema kwamba hujaonekana huko, Ahabu alimtaka huyo mfalme aape na watu wake kwamba kweli hupo.

11. Na sasa, wataka niende kumwambia kwamba wewe uko hapa!

12. Ninahofia kwamba mara nitakapoondoka, Roho ya Mwenyezi-Mungu itakunyakua na kukupeleka mahali nisipopajua! Nikienda kumwambia Ahabu kwamba uko hapa, naye akikutafuta asikupate, ataniua mimi, ingawaje mimi mtumishi wako nimemcha Mwenyezi-Mungu tangu ujana wangu.

13. Je, huna habari kwamba Yezebeli alipokuwa akiwaua manabii wa Mwenyezi-Mungu, mimi niliwaficha manabii 100, watu hamsinihamsini pangoni, nikawa nawapa chakula na maji?

14. Sasa waniambia ati niende kumwambia bwana wangu kwamba wewe Elia uko hapa! Ahabu ataniua.”

15. Elia akamwambia, “Nakuapia kwa jina la Mwenyezi-Mungu wa Majeshi, aishivyo ambaye ninamtumikia: Leo hii nitajitokeza mbele ya mfalme.”

Kusoma sura kamili 1 Wafalme 18