Agano la Kale

Agano Jipya

1 Wafalme 18:23-34 Biblia Habari Njema (BHN)

23. Haya! Leteni fahali wawili; manabii wa Baali wajichagulie fahali mmoja, wamchinje, wamkate vipandevipande na kumweka juu ya kuni, bila kuwasha moto. Nami pia nitamtwaa huyo fahali mwingine, nitamchinja na kumweka juu ya kuni bila kuwasha moto.

24. Kisha, wao watamwomba mungu wao, nami nitamwomba Mwenyezi-Mungu. Mungu atakayejibu kwa kuleta moto, huyo ndiye Mungu wa kweli.” Na hapo umati wote ukasema, “Naam! Na iwe hivyo.”

25. Kisha, Elia akawaambia manabii wa Baali, “Nyinyi ni wengi; basi anzeni. Jichagulieni fahali, mtayarisheni na kumwomba mungu wenu, lakini msiwashe moto.”

26. Hao manabii wakamtwaa fahali wao waliyepewa, wakamtayarisha, kisha wakaanza kumlilia Baali kutoka asubuhi hadi adhuhuri, wakirukaruka na kuyumbayumba kuizunguka madhabahu waliyotengeneza wakisema: “Ee Baali, utusikie!” Lakini hapakutokea sauti yoyote, wala hakuna aliyewajibu.

27. Ilipofika saa sita mchana, Elia akaanza kuwadhihaki akisema, “Ombeni kwa sauti kubwa zaidi! Yeye ni mungu ati! Huenda ikawa amezama katika mawazo yake, amekwenda haja, au yumo safarini! Labda amelala, mnapaswa kumwamsha!”

28. Manabii hao wakapiga kelele zaidi, wakajikatakata kwa visu na simi, kufuatana na desturi yao, hata wakabubujika damu.

29. Wakaendelea kupiga makelele na kufanya kama wendawazimu hadi alasiri wakati wa kutoa tambiko; lakini hakuna aliyewajibu wala kuwajali.

30. Basi, Elia akawaambia watu, “Sogeeni karibu nami.” Wao wakamkaribia. Kisha Elia akaijenga upya madhabahu ya Mwenyezi-Mungu iliyokuwa imebomolewa.

31. Alitwaa mawe kumi na mawili, hesabu ya makabila kumi na mawili yaliyopewa majina ya wana wa Yakobo ambaye Mwenyezi-Mungu alimwambia “Jina lako litakuwa Israeli.”

32. Kwa mawe hayo, Elia alimjengea Mwenyezi-Mungu madhabahu, akachimba na mtaro kuizunguka madhabahu hiyo; mtaro uwezao kuchukua kama debe moja na nusu la nafaka.

33. Kisha akapanga kuni vizuri, akamkata vipandevipande yule fahali, akaviweka juu ya kuni. Kisha akawaambia watu, “Jazeni mitungi minne maji mkaimwagie tambiko hii ya kuteketezwa pamoja na kuni.” Wakafanya hivyo.

34. Kisha akawaambia, “Rudieni tena.” Nao wakafanya hivyo mara ya pili. Naye akawaambia, “Fanyeni hivyo tena mara ya tatu.” Nao wakafanya hivyo.

Kusoma sura kamili 1 Wafalme 18