Agano la Kale

Agano Jipya

1 Wafalme 16:19-29 Biblia Habari Njema (BHN)

19. Jambo hilo lilifanyika kwa sababu ya dhambi alizotenda alifanya maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, akamwiga Yeroboamu na kuwafanya watu wa Israeli watende dhambi.

20. Matendo mengine ya Zimri na njama aliyokula, yote yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Israeli.

21. Watu wa Israeli, sasa, waligawanyika makundi mawili: Kundi moja lilimtambua Tibni mwana wa Ginathi kuwa mfalme, na kundi la pili lilimtambua Omri.

22. Hatimaye watu wa kundi lililomtambua Omri, wakawazidi nguvu wale waliomtambua Tibni mwanawe Ginathi; Tibni akafa na Omri akawa mfalme.

23. Omri alianza kutawala mnamo mwaka wa thelathini na mmoja wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda. Alitawala kwa muda wa miaka kumi na miwili; miaka sita alikuwa anatawala kutoka mjini Tirza.

24. Alinunua mlima wa Samaria kwa vipande 6,000 vya fedha kutoka kwa mtu mmoja aitwaye Shemeri, akajenga ngome juu yake, na mji. Mji wenyewe akauita Samaria, kwa heshima ya Shemeri aliyeumiliki mlima huo hapo awali.

25. Omri alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu; alifanya maovu zaidi ya wale wote waliomtangulia.

26. Kwa sababu alimwiga Yeroboamu mwana wa Nebati, akamkasirisha Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kwa kuwafanya watu wa Israeli watende dhambi kwa kuabudu sanamu za miungu.

27. Matendo mengine ya Omri na ushujaa wake, yote yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Israeli.

28. Hatimaye, Omri alifariki, akazikwa huko Samaria; mwanawe Ahabu akatawala mahali pake.

29. Mnamo mwaka wa thelathini na nane wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda, Ahabu mwana wa Omri, alianza kutawala Israeli. Alitawala huko Samaria kwa muda wa miaka ishirini na miwili.

Kusoma sura kamili 1 Wafalme 16