Agano la Kale

Agano Jipya

1 Wafalme 15:16-32 Biblia Habari Njema (BHN)

16. Mfalme Asa wa Yuda, na mfalme Baasha wa Israeli, walikuwa na vita kati yao wakati wote walipokuwa wakitawala.

17. Baasha, mfalme wa Israeli, aliishambulia nchi ya Yuda na kuanza kuujenga Rama ili apate kuzuia mtu yeyote asitoke wala asiingie kwa Asa, mfalme wa Yuda.

18. Ndipo mfalme Asa akachukua fedha na dhahabu yote iliyobaki katika hazina ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu na katika hazina ya ikulu, akawapa watumishi wake, akawatuma Damasko kwa Ben-hadadi mwana wa Tabrimoni, mjukuu wa Hezioni, mfalme wa Aramu, akasema,

19. “Tufanye mkataba wa ushirikiano kati yangu na wewe kama vile walivyofanya baba yangu na baba yako; tazama, nimekupelekea zawadi ya fedha na dhahabu; nenda ukavunje mkataba wa ushirikiano ulioko kati yako na mfalme Baasha wa Israeli, ili aache mashambulizi dhidi yangu.”

20. Hapo mfalme Ben-hadadi akakubali pendekezo la mfalme Asa, akawatuma majemadari wake na majeshi yake kwenda kuishambulia miji ya Israeli. Nao wakateka Iyoni, Dani, Abel-beth-maaka, Kinerethi yote, na nchi yote ya Naftali.

21. Mfalme Baasha alipopata habari za mashambulizi hayo aliacha kuujenga mji wa Rama akaishi katika Tirza.

22. Ndipo mfalme Asa alipotoa tangazo kwa watu wote wa Yuda, bila kumwacha hata mtu mmoja, wahamishe mawe ya Rama na mbao, vifaa ambavyo Baasha alivitumia kujengea. Kisha mfalme Asa alitumia vifaa hivyo kujengea Geba, katika Benyamini na Mizpa.

23. Matendo mengine yote ya Asa, ushujaa wake na miji yote aliyoijenga, yote yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Yuda. Lakini, wakati wa uzee wake, Asa alishikwa na ugonjwa wa miguu.

24. Hatimaye, Asa alifariki, akazikwa katika makaburi ya kifalme, katika mji wa Daudi, naye mwanawe Yehoshafati akatawala mahali pake.

25. Mnamo mwaka wa pili wa utawala wa Asa huko Yuda, Nadabu, mwana wa Yeroboamu, alianza kutawala huko Israeli. Alitawala kwa muda wa miaka miwili.

26. Nadabu alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu; akamwiga baba yake ambaye aliwafanya watu wa Israeli watende dhambi.

27. Baasha mwana wa Ahiya, wa kabila la Isakari, akala njama dhidi ya Nadabu. Basi, wakati Nadabu na jeshi lake walipokuwa wameuzingira mji wa Gibethoni wa Wafilisti, Baasha akamvamia na kumwua,

28. akatawala mahali pake. Huo ulikuwa mwaka wa tatu wa utawala wa mfalme Asa wa Yuda.

29. Mara tu alipoanza kutawala, Baasha akawaua watu wote wa jamaa ya Yeroboamu; hakuacha hai hata mtu mmoja wa jamaa ya Yeroboamu; hiyo ilikuwa sawa na yale aliyosema Mwenyezi-Mungu kwa njia ya mtumishi wake, Ahiya wa Shilo.

30. Mambo haya yalifanyika kwa sababu Yeroboamu alimkasirisha Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kwa dhambi yake na kwa kuwafanya watu wa Israeli watende dhambi.

31. Matendo mengine ya Nadabu, yote yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Israeli.

32. Mfalme Asa wa Yuda na mfalme Baasha wa Israeli walikuwa na vita kati yao wakati wote walipokuwa wakitawala.

Kusoma sura kamili 1 Wafalme 15