Agano la Kale

Agano Jipya

1 Samueli 4:13-22 Biblia Habari Njema (BHN)

13. Eli, akiwa na wasiwasi moyoni kuhusu sanduku la Mungu, alikuwa ameketi kwenye kiti chake, kando ya barabara akiangalia. Yule mtu alipowasili mjini na kueleza habari hizo, mji mzima ulilia kwa sauti.

14. Eli aliposikia sauti ya kilio, akauliza, “Kelele hizo ni za nini?” Yule mtu akaenda haraka kwa Eli ili kumpa habari hizo.

15. Wakati huo, Eli alikuwa na umri wa miaka tisini na nane na macho yake yalikuwa yamepofuka.

16. Yule mtu akamwambia Eli, “Mimi nimetoka vitani sasa hivi; nimekimbia kutoka vitani leo.” Eli akamwuliza, “Mwanangu, mambo yalikuwaje huko?”

17. Yule aliyeleta habari akasema, “Waisraeli wamewakimbia Wafilisti. Kumekuwa na mauaji makubwa miongoni mwa Waisraeli. Zaidi ya yote, wanao wote wawili, Hofni na Finehasi, wameuawa, na sanduku la agano la Mungu limetekwa.”

18. Huyo mtu alipotaja tu sanduku la Mungu, Eli alianguka chali kutoka kwenye kiti chake kando ya lango. Eli alipoanguka hivyo, shingo yake ilivunjika kwani alikuwa mzee na mnene, naye akafariki. Eli alikuwa mwamuzi wa Israeli kwa muda wa miaka arubaini.

19. Tena ilitokea kwamba, mkwewe Eli, yaani mke wa Finehasi, wakati huo alikuwa mjamzito, na muda wake wa kujifungua ulikuwa umekaribia. Aliposikia kwamba sanduku la agano la Mungu limetekwa na kwamba baba mkwe wake, hata na mumewe wamefariki, mara moja alipata utungu, na kujifungua.

20. Basi, alipokuwa anakufa, wanawake waliokuwa wanamsaidia walimwambia, “Usiogope, maana umejifungua mtoto wa kiume.” Lakini yeye hakujibu neno, wala hakuwasikiliza.

21. Naye akamwita mtoto wake Ikabodi, akimaanisha, “Utukufu wa Mungu umeondoka Israeli,” akiwa na maana kwamba sanduku la agano lilikuwa limetekwa, tena baba mkwe wake na mumewe, wote walifariki.

22. Akasema, “Utukufu wa Mungu umeondoka Israeli kwani sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu limetekwa.”

Kusoma sura kamili 1 Samueli 4