Agano la Kale

Agano Jipya

1 Samueli 30:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Siku ya tatu baadaye, Daudi na watu wake wakarudi Siklagi. Waamaleki walikuwa wamekwisha shambulia Negebu pamoja na mji wa Siklagi na kuuteketeza kwa moto.

2. Walikuwa wameteka wanawake na watu wote waliokuwa mjini humo, wakubwa kwa wadogo. Hao waliowateka, waliondoka nao wakiwa hai, bila ya kumwua mtu yeyote.

3. Daudi na watu wake walipofika mjini waliukuta mji umeteketezwa, na wanawake, watoto wao wa kiume na wa kike, wamechukuliwa mateka.

4. Ndipo Daudi na watu wake walipoangua kilio, wakalia hadi walipoishiwa nguvu.

5. Wake wawili wa Daudi, Ahinoamu kutoka Yezreeli na Abigaili mjane wa Nabali, nao pia walikuwa wamechukuliwa mateka.

6. Sasa, Daudi alikuwa katika matatizo makubwa kwa kuwa watu wake walikuwa na uchungu rohoni mwao kwa kupoteza watoto wao; hivyo wakawa wanamtishia kumpiga mawe. Lakini Daudi alijipa moyo kwa kumtegemea Mwenyezi-Mungu, Mungu wake.

7. Daudi akamwambia kuhani Abiathari mwana wa Ahimeleki, “Niletee kizibao cha kuhani.” Abiathari akampelekea.

8. Daudi akamwomba Mwenyezi-Mungu shauri, “Je, genge hili nilifuate? Na je nitalikamata?” Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Lifuate kwani utalipata na kuwaokoa hao waliotekwa.”

9. Kwa hiyo, Daudi akaondoka pamoja na wale watu 600 aliokuwa nao. Walipofika kwenye kijito cha Besori, wakawakuta baadhi ya watu waliotekwa wameachwa hapo.

10. Lakini Daudi aliendelea kulifuatilia lile genge akiwa na watu 400, watu 200 wakabaki hapo kwani walichoka mno, wasiweze kuvuka kijito hicho.

11. Wale watu waliokuwa na Daudi walimkuta mtu mmoja Mmisri nyikani, nao wakampeleka kwa Daudi. Wakampa mtu huyo mkate na maji.

12. Pia walimpa kipande cha mkate wa tini na vishada viwili vya zabibu kavu. Alipomaliza kula, akapata nguvu, kwani alikuwa hajala wala kunywa kitu chochote kwa muda wa siku tatu, mchana na usiku.

Kusoma sura kamili 1 Samueli 30