Agano la Kale

Agano Jipya

1 Samueli 28:16-24 Biblia Habari Njema (BHN)

16. Samueli akasema, “Kwa nini unaniomba shauri ambapo Mwenyezi-Mungu amekupa kisogo na amekuwa adui yako?

17. Mwenyezi-Mungu amekutendea kile alichokuambia kwa njia yangu. Mwenyezi-Mungu ameurarua ufalme kutoka mikononi mwako, na amempa Daudi jirani yako.

18. Maana, wewe hukuitii sauti ya Mwenyezi-Mungu, wala hukuitekeleza ghadhabu yake dhidi ya Waamaleki. Ndio maana leo Mwenyezi-Mungu amekutendea mambo haya.

19. Zaidi ya hayo, Mwenyezi-Mungu atakutia wewe pamoja na Waisraeli wote mikononi mwa Wafilisti. Kesho, wewe na wanao mtakuwa pamoja nami; hata jeshi la Israeli Mwenyezi-Mungu atalitia mikononi mwa Wafilisti.”

20. Ghafla, Shauli akiwa na hofu kutokana na maneno ya Samueli, alianguka kifudifudi; hakuwa na nguvu zozote; kwa kuwa alikuwa hajala chochote kwa siku nzima, usiku na mchana.

21. Ndipo yule mwanamke alipomwendea Shauli, na alipoona kuwa Shauli ameshikwa na hofu mno, alimwambia, “Mimi mtumishi wako nimehatarisha maisha yangu kwa kufanya kile ulichoniambia nikufanyie.

22. Sasa, nisikilize mimi mtumishi wako; nitakuandalia mkate ili ule nawe utakuwa na nguvu za kuendelea na safari yako.”

23. Lakini Shauli alikataa na kusema, “Sitakula.” Lakini watumishi pamoja na yule mwanamke, walimsihi ale, naye akawasikiliza. Hivyo aliinuka kutoka chini na kukaa kwenye kitanda.

24. Yule mwanamke alikuwa na ndama wake mmoja nyumbani aliyenona, akamchinja haraka, akachukua unga wa ngano, akaukanda, akatengeneza mkate usiotiwa chachu.

Kusoma sura kamili 1 Samueli 28