Agano la Kale

Agano Jipya

1 Samueli 26:8-19 Biblia Habari Njema (BHN)

8. Abishai akamwambia Daudi, “Leo Mungu amemtia adui yako mikononi mwako. Basi, niache nimbane udongoni kwa pigo moja tu la mkuki; sitampiga mara mbili.”

9. Lakini Daudi akamwambia Abishai, “Usimwangamize; maana hakika Mwenyezi-Mungu atamwadhibu mtu yeyote atakayeunyosha mkono wake dhidi ya mteule wake aliyepakwa mafuta.

10. Naapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai, kwamba Mwenyezi-Mungu mwenyewe atamuua Sauli; ama siku yake ya kufa itafika, au atakwenda vitani na kufia huko.

11. Lakini Mwenyezi-Mungu anakataza nisinyoshe mkono wangu dhidi ya mtu ambaye amemteua kwa kumpaka mafuta. Lakini chukua mkuki wake ulio karibu na kichwa chake pamoja na gudulia lake la maji, halafu tujiendee zetu.”

12. Hivyo, Daudi alichukua ule mkuki na gudulia la maji karibu na kichwa cha Shauli nao wakajiendea zao. Lakini hakuna mtu aliyeona au kujua tukio hilo, wala hakuna aliyeamka, kwa kuwa Mwenyezi-Mungu aliwaletea usingizi mzito.

13. Kisha, Daudi akaenda upande wa pili wa bonde hilo, akasimama juu mlimani mbali na kundi la Shauli.

14. Akaliita kwa sauti jeshi la Shauli na Abneri mwana wa Neri akisema, “Abneri, je, unanisikia?” Abneri akauliza, “Ni nani wewe unayemwita mfalme?”

15. Daudi akamjibu, “Je, wewe si mwanamume? Nani aliye sawa nawe katika Israeli? Mbona basi, hukumlinda bwana wako mfalme? Mtu mmoja wetu aliingia hapo kumwangamiza bwana wako mfalme!

16. Ulilotenda si jambo jema. Ninaapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai, kwamba unastahili kufa, kwa kuwa hukumlinda bwana wako, ambaye Mwenyezi-Mungu amempaka mafuta. Sasa hebu angalia, mkuki wa mfalme na lile gudulia la maji lililokuwa karibu na kichwa chake kama vipo!”

17. Shauli alitambua sauti ya Daudi, akamwuliza, “Je, hiyo ni sauti yako mwanangu Daudi?” Daudi akamjibu, “Bwana wangu, mfalme, ni sauti yangu.”

18. Halafu akaendelea kusema, “Lakini kwa nini, wewe bwana wangu unifuatilie mimi mtumishi wako? Nimefanya nini? Ni ovu gani nimekufanyia?

19. Basi, sasa bwana wangu mfalme, usikie maneno ya mtumishi wako. Ikiwa Mwenyezi-Mungu ndiye aliyekuchochea uje dhidi yangu, basi, na apokee tambiko itakayomfanya abadili nia yake. Lakini kama ni watu, basi, Mwenyezi-Mungu na awalaani watu hao kwani wamenifukuza kutoka urithi aliotupa Mwenyezi-Mungu wakisema, ‘Nenda ukaitumikie miungu mingine.’

Kusoma sura kamili 1 Samueli 26