Agano la Kale

Agano Jipya

1 Samueli 26:13-25 Biblia Habari Njema (BHN)

13. Kisha, Daudi akaenda upande wa pili wa bonde hilo, akasimama juu mlimani mbali na kundi la Shauli.

14. Akaliita kwa sauti jeshi la Shauli na Abneri mwana wa Neri akisema, “Abneri, je, unanisikia?” Abneri akauliza, “Ni nani wewe unayemwita mfalme?”

15. Daudi akamjibu, “Je, wewe si mwanamume? Nani aliye sawa nawe katika Israeli? Mbona basi, hukumlinda bwana wako mfalme? Mtu mmoja wetu aliingia hapo kumwangamiza bwana wako mfalme!

16. Ulilotenda si jambo jema. Ninaapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai, kwamba unastahili kufa, kwa kuwa hukumlinda bwana wako, ambaye Mwenyezi-Mungu amempaka mafuta. Sasa hebu angalia, mkuki wa mfalme na lile gudulia la maji lililokuwa karibu na kichwa chake kama vipo!”

17. Shauli alitambua sauti ya Daudi, akamwuliza, “Je, hiyo ni sauti yako mwanangu Daudi?” Daudi akamjibu, “Bwana wangu, mfalme, ni sauti yangu.”

18. Halafu akaendelea kusema, “Lakini kwa nini, wewe bwana wangu unifuatilie mimi mtumishi wako? Nimefanya nini? Ni ovu gani nimekufanyia?

19. Basi, sasa bwana wangu mfalme, usikie maneno ya mtumishi wako. Ikiwa Mwenyezi-Mungu ndiye aliyekuchochea uje dhidi yangu, basi, na apokee tambiko itakayomfanya abadili nia yake. Lakini kama ni watu, basi, Mwenyezi-Mungu na awalaani watu hao kwani wamenifukuza kutoka urithi aliotupa Mwenyezi-Mungu wakisema, ‘Nenda ukaitumikie miungu mingine.’

20. Usiniache nife katika nchi ya kigeni, mbali na Mwenyezi-Mungu. Kwa nini wewe mfalme wa Israeli umetoka kuyatafuta maisha yangu kama mtu anayewinda kware milimani?”

21. Ndipo Shauli akajibu, “Mimi nimefanya makosa. Rudi mwanangu Daudi. Sitakudhuru tena kwa kuwa leo maisha yangu yalikuwa ya thamani mbele yako. Mimi nimekuwa mpumbavu na nimekosa vibaya sana.”

22. Daudi akajibu, “Ee mfalme, mkuki wako uko hapa, mtume kijana wako mmoja aje auchukue.

23. Mwenyezi-Mungu humtunza kila mtu kwa uadilifu na uaminifu wake. Leo Mwenyezi-Mungu alikutia mikononi mwangu, lakini mimi sikunyosha mkono wangu dhidi yako kwa kuwa wewe umeteuliwa naye kwa kutiwa mafuta.

24. Tazama kama vile leo maisha yako yalivyokuwa na thamani mbele yangu, ndivyo na maisha yangu yawe na thamani mbele ya Mwenyezi-Mungu; naye akaniokoe kutoka kwenye taabu zote.”

25. Shauli akamwambia Daudi, “Mungu na akubariki mwanangu Daudi. Utafanya mambo makuu, nawe utafanikiwa katika yote.” Basi, Daudi akaenda zake; Shauli naye akarudi nyumbani kwake.

Kusoma sura kamili 1 Samueli 26