Agano la Kale

Agano Jipya

1 Samueli 25:23-37 Biblia Habari Njema (BHN)

23. Abigaili alipomwona tu Daudi, akashuka mara moja kutoka juu ya punda wake, na kuinama mbele ya Daudi hadi uso wake ukagusa chini.

24. Alijitupa miguuni pa Daudi na kumwambia, “Bwana wangu, hatia yote na iwe juu yangu tu. Nakuomba niongee nawe mimi mtumishi wako. Nakuomba usikilize maneno ya mtumishi wako.

25. Usimfikirie Nabali ambaye ni mtu mbaya kwani lilivyo jina lake Nabali, ndivyo naye alivyo. Yeye anaitwa Nabali; na kweli yeye ni mtu mpumbavu. Bwana wangu, wale vijana wako ulipowatuma, mimi mtumishi wako sikuwaona.

26. Sasa bwana wangu, naapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai, na vile ulivyo hai, kwamba kwa kuwa Mwenyezi-Mungu amekuzuia usilipize kisasi kwa kumwaga damu na kujipatia lawama, waache adui zako na wale wote wanaokutakia mabaya wawe wapumbavu kama Nabali.

27. Bwana wangu, nakuomba upokee zawadi hii niliyokuletea, na uwape vijana wanaokufuata.

28. Nakuomba unisamehe mimi mtumishi wako. Mwenyezi-Mungu atakupa jamaa imara kwa sababu, wewe bwana wangu, unapigana vita vya Mwenyezi-Mungu. Wakati wote wa maisha yako usipatikane na baa lolote.

29. Kukitokea watu wakikufuatilia na kutaka kuyaangamiza maisha yako, Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, atayasalimisha maisha yako pamoja na walio hai. Lakini maisha ya adui zako atayatupilia mbali, kama vile mtu atupavyo jiwe kwa kombeo.

30. Baada ya Mwenyezi-Mungu kukutendea mema yote aliyokuahidi, na kukuteua kuwa mtawala wa Israeli,

31. wewe bwana wangu, hutakuwa na sababu ya kujuta wala kuhukumiwa na dhamiri kutokana na kumwaga damu bila sababu kwa kujilipiza kisasi. Lakini, bwana wangu, Mwenyezi-Mungu atakapokuwa amekutendea wema huo, nakuomba unikumbuke mimi mtumishi wako.”

32. Daudi akamwambia Abigaili, “Atukuzwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, aliyekutuma leo kukutana nami.

33. Mtukuze Mwenyezi-Mungu aliyekupa busara kwa kunizuia kuwa na hatia ya umwagaji damu na kujilipiza kisasi mimi mwenyewe.

34. Kwa hakika, Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, amenizuia nisikudhuru. Usingefanya haraka kuja kukutana nami, kwa hakika, kesho asubuhi hakuna mwanamume yeyote wa Nabali angesalia.”

35. Kisha, Daudi akapokea vitu vyote ambavyo Abigaili alikuwa amemletea, akamwambia Abigaili, “Rudi nyumbani kwako kwa amani. Tazama, mimi nimeyasikia uliyoyasema, na ombi lako nimelipokea.”

36. Abigaili aliporudi nyumbani, alimkuta Nabali akifanya karamu kubwa nyumbani kwake kama ya kifalme. Nabali alikuwa ameburudika sana moyoni kwani alikuwa amelewa sana. Hivyo hakumwambia lolote mpaka asubuhi.

37. Asubuhi, Abigaili alipoona mumewe divai imemtoka, alimweleza mambo yote, na papo hapo Nabali akapooza, akawa kama jiwe.

Kusoma sura kamili 1 Samueli 25