Agano la Kale

Agano Jipya

1 Samueli 23:5-16 Biblia Habari Njema (BHN)

5. Basi, Daudi akaenda Keila pamoja na watu wake, na huko akapigana na Wafilisti, akawaua Wafilisti wengi na kuteka nyara ng'ombe wengi. Hivyo Daudi aliwaokoa wakazi wa Keila.

6. Abiathari, mwana wa Ahimeleki, alipokimbilia kwa Daudi huko Keila, alikwenda na kizibao cha kuhani.

7. Shauli alipoambiwa kuwa Daudi amekwisha fika Keila, akasema, “Mungu amemtia mikononi mwangu kwani amejifungia mwenyewe kwa kuingia katika mji wenye malango yenye makomeo.”

8. Hivyo, Shauli aliyaita majeshi yaende Keila na kufanya mashambulizi, ili kumzingira Daudi pamoja na watu wake.

9. Daudi aliposikia mipango miovu ya Shauli dhidi yake, akamwambia kuhani Abiathari, “Kilete hapa hicho kizibao cha kuhani.”

10. Kisha Daudi akaomba, “Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kwa hakika mimi mtumishi wako, nimesikia kwamba Shauli anapanga kuja kuangamiza mji wa Keila kwa sababu yangu.

11. Je, wakazi wa Keila watanitia mikononi mwa Shauli? Je, Shauli atakuja kweli kama nilivyosikia mimi mtumishi wako? Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, nakuomba unijibu mimi mtumishi wako.”Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Shauli atakuja.”

12. Daudi akamwuliza, “Je, wakazi wa Keila watanitia mikononi mwa Shauli, mimi pamoja na watu wangu?” Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Watakutia mikononi mwake.”

13. Kisha, Daudi na watu wake ambao walikuwa kama 600, waliondoka na kwenda popote walipoweza kwenda. Shauli aliposikia kwamba Daudi amekwisha kimbia kutoka Keila, akaiacha mipango yake yote.

14. Basi, Daudi alibaki ngomeni jangwani, katika nchi ya milima ya mbuga za Zifu. Shauli alimtafuta kila siku, lakini Mungu hakumtia Daudi mikononi mwa Shauli.

15. Daudi alijua kuwa Shauli alitaka kuyaangamiza maisha yake. Daudi akawa katika mbuga za Zifu, huko Horeshi.

16. Yonathani mwana wa Shauli alimfuata Daudi huko Horeshi akamtia moyo kwamba Mungu anamlinda.

Kusoma sura kamili 1 Samueli 23